Mtwara. Wafanyakazi zaidi
ya 360 wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara, wamekamatwa kwa kufanya
kazi nchini bila kuwa na vibali vya Uhamiaji.
Kamatakamata
hiyo imekuja baada ya agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga la
kuwakamata wahamiaji haramu na wageni wanaofanya kazi bila vibali.
Jana,
ofisi ya Uhamiaji ya mkoa ilifanya operesheni katika kiwanda hicho, lakini
haikupewa ushirikiano na uongozi.
Ofisa
Uhamiaji wa mkoa, Zakayo Mchele alisema walifika kiwandani hapo kufanya
ukaguzi, lakini walikosa ushirikiano kutoka kwa Meneja Mkuu aliyefahamika kwa
jina la Vidya Digixt.
Mchele
alisema kutokana na meneja huyo kutotoa ushirikiano, wanamshikilia ili
kusaidiana na Uhamiaji kuwabaini wafanyakazi wanaoishi bila uhalali na pia
watamfikisha mahakamani.
Alisema
licha ya kukosa ushirikiano, wafanyakazi 117 wa kiwanda hicho walipeleka maombi
ya kutaka kupewa vibali vya kazi.
Mchele
alisema walifanya msako katika mpaka wa Kilambo na Wilaya ya Tandahimba na
kuwakamata watu 48 raia wa Ethiopia ambao walisafirishwa kwa malori kutoka
Kenya.
“
Pia, tuliwakamata raia wengine wawili wa Msumbiji wakiwa na kadi za kupigia
kura (za Tanzania) na kukamatwa siyo kwamba msako ulikuwa haufanyiki siku za
nyuma,” alisema.
Alisema
mwaka jana idadi ya watu walioingia nchini bila kibali kwa Mkoa wa Mtwara
walikuwa 121. Ofisa
huyo alisema katika operesheni hiyo kesi zilizopelekwa mahakamani ni 36 ambazo
zilikamilika na wahusika kutiwa hatiani na kutozwa faini, huku wengine wakipewa
adhabu ya kutumikia kifungo.
No comments:
Post a Comment