Kaimu Mkurugenzi Mkuu Wa TAKUKURU Atangaza Kiama Kwa Wala Rushwa Hasa Watumishi Wa Umma
TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), imetoa onyo kwa
taasisi nyeti nne hapa nchini ikiwemo wanaohusika na matumizi ya fedha
za Umma kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Pia,Takukuru
inashughulikia kukamilisha kesi kubwa 36, zinazowahusu watumishi wenye
ushawishi na hadhi kubwa hapa nchini ambapo kati ya hizo zipo
zilizokamilika na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam leo , Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo,
Valentino Mlowola alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kwa wananchi
kuwajulisha matendo ya rushwa na ufisadi yanayoendelea hapa nchini.
Alisema
kutokana na hali ya wananchi kuona nia ya serikali ya awamu ya tano
katika kushughulikia matatizo ya rushwa na ufisadi hapa nchini ametoa onyo kwa maofisa wa umma wanaofanya rushwa na ufisadi kuwa sehemu yao ya kazi na miradi ya kuwaingizia kipato.
“Natoa
onyo kwa maofisa wa umma ambao wamefanya rushwa na ufisadi kuwa ni
sehemu ya kazi zao na miradi ya kuwaingizia kipato, wajitafakari kabla
hawajaamua kujihusisha na vitendo vya rushwa,”alisema.
Alisema
hawatasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watumishi
watakaojiingiza katika kulihujumu taifa na wananchi kwani wananchi
wanakiu ya kupata maendeleo na maisha bora na kuwataka watambue wananchi
wa jana si wa leo kwani wamedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali
yao.
Mlowola alitoa onyo
kwa maofisa maduhuli na watekelezaji wa jukumu la kukusanya kodi za
wananchi kwa kutomuonea mtu haya kwa atakayejihusisha na ubadhirifu wa
fedha na mali ya umma.
“Wakusanye
kodi halali ya serikali kwa kufuata sheria, taratibu na Kanuni
zinazowaongoza kukusanya kodi, tutachukua hatua stahiki pale
kutakapokuwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo,”alisema.
Pia, Mlowola alitoa onyo
kwa watakaohusika kwenye matumizi ya fedha za umma kwamba wafuate
sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza kwani taasisi hiyo
haitawavumilia watakaokiuka fedha za serikali isiyo halali.
Mbali
na hilo, pia Kaimu huo alitoa onyo kwa watumishi wa umma wenye jukumu
la kuhudumia mahitaji ya umma kwa kutojihusisha na rushwa kwa kutekeleza
majukumu yao katika muda uliotakiwa, weledi na uaminifu.
Alisema
taasisi hiyo haipo kwa lengo la maslahi ya watu wabadhilifu wa mali ya
umma kwani uchunguzi wa kesi ya kuisababishia hasara serikali shilingi bilioni 8.5 kutokana na ukwepaji wa kodi wa kampuni ya Mafuta ya Lake Oil kwa kufanya udanganyifu wa kuuza mafuta ndani ya nchi Petrol lita 17,461,111.58 kwa kudanganya zilisafirishwa umefikia hatua nzuri.
“Takukuru imekamilisha shauri hili na mtuhumiwa wamepewa miezi miwili kurejesha mikononi fedha zote .Tutawarudisha mahakamani endapo watashindwa kurejesha kiasi hicho,”alisema.
Alisema
mbali na shauri hilo, wapo kwenye hatua nzuri ya kukamilisha ya
uchunguzi wa kesi ya hati fungani ya malipo yaliyolipwa na kampuni ya
Enterprise Growth Markert Advisor(EGMA), kiasi cha dola 6,000,000 kwa
lengo la kuisaidai Tanzania kupata mkopo wa dola 600,000,000.
“Takukuru
imebaini fedha hizo dola 6,000,000 zilitakatishwa na watumishi wa umma
wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi kutoka sekta binafsi huku
wakijua fedha hizo wamezipata kwa njia haramu,”alisema.
Akizungumzia
hatua aliyochukua rais, Dk. John Magufuli kwa kutengua uteuzi wa
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Mhandisi Benhadard Tito kwa tuhuma
zinazomkabili tayari wanachunguza shirika hilo la reli.
Alisema
kulikuwepo na ukiukwaji wa kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya
kisasa ya kimataifa(Standard Gauge) unaosimamiwa na Shirika la Hodhi la
Reli Nchini(RAHCO), watuhumiwa wamekamatwa akiwemo raia wa Kenya aliyekuwa kwenye mchakato huo, Kanji Muhando.
Kaimu
huyo alisema shauri la kesi ya mabehewa ya kokoto 25 ya shirika la
reili nchini (TRL), ya kukiuka sheria ya manunuzi ya umma Na.21/2004
pamoja na kanuni zake kutoka kampuni ya Hindustha Engineering and
Industries Limited limekamilika.
“Uchunguzi
umekamilika na tumeshapeleka kwa mkurugenzi wa Mashtaka kuomba kibali
cha kuwafikisha watuhumiwa waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa
na ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa umma
mahakamani,”alisema.
Alisema
rais alijipa kazi ya kutumbua majipu hivyo aliwasihi watumishi wa
taasisi hiyo kutumikia wananchi kwa weledi huku akibainisha tayari
wanatekeleza azma na dhamira ya rais ya kupambana na rushwa.
Akitolea
ufafanuzi swala la kumsubiri rais kutumbua majipu ndio taasisi hiyo
ifanye ufafanuzi, Mlowola alisema taasisi hiyo imejipanga vilivyo tangu
Novemba 20 mwaka jana wakati rais alipohutubia bungeni alipoonesha
dhamira na nia ya dhati ya kupambana na rushwa na ufisadi bila kumuonea
mtu haya.
“Nitoe
rai kwa wananchi kutoa taarifa ili tuweze kujua kabla hatujapigwa,
tukiweza kuisaidia serikali kuokoa fedha kabla hatujapigwa zitasaidia
wananchi kutoa elimu bure, upatikanaji wa dawa na mishahara mizuri,”alisema.
Alisema
tayari wameshaanza kuchunguza madai ya aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kwani tayari wapo hata viongozi
wakubwa.
Akizungumzia
maofisa takukuru waliofukuzwa kazi a rais baada ya kukiuka maagizo ya
rais ya kupata kibali cha kusafiri nje, alisema maofisa hao walikwenda
kwenye mkutano wa taasisi za kupambana na rushwa uliofanyika Congo-Kinshasa.
No comments:
Post a Comment