Muda mfupi baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kasoro na athari za kurudia Uchaguzi uliofutwa kinyume cha sheria na Jecha Salim Jecha, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametangaza kuwa uchaguzi huo lazima urudiwe.
Wakizungumza jana na vijana wa chama cha Mapinduzi katika viwanja vya Maisara waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya matembezi ya kuunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar,viongozi wa juu wa chama hicho walisisitiza kuwa uchaguzi wa Zanzibar upo pale pale na utarudiwa kadiri tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) itakavyotangaza.
Wa kwanza kutoa msimamo huo alikuwa ni Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, aliyesema kuwa uchaguzi huo utarudiwa hata ikiwezekana vyama vyote vikijitoa CCM kitashiriki peke yake
“Uchaguzi wa marudio upo pale pale, tunajua uchaguzi ulifutwa kihalali, mjitayarishe kwa uchaguzi wa marudio. CUF wamesema watatumia nguvu ya umma, tunawakaribisha na wataona matokeo yake” alisema Balozi Iddi.
Katika mkutano huo uliokuwa unarushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha ZBC, Dk Alli Mohamed Shein alipongeza msimamo wa Balozi Iddi, na kusema atabaki kuwa rais hadi uchaguzi utakaporudiwa.
Dk Shein alisema yupo madarakani kwa kushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwamba hajavunja katiba na kama itatokea mahakama ikatoa ufafanuzi kuwa anakosea kuwepo hapo kikatiba basi ataondoka madarakani
“Mahakama ikisema nakosea nitaondoka, Rais yupo Baraza la Mapinduzi lipo na Mawaziri wapo, nitaita waandishi wa habari Ikulu na mimi nimjibu Maalim Seif kwani kuna mengi amenisingizia” alisema.
No comments:
Post a Comment