Friday, January 8, 2016

CHADEMA WAJICHIMBIA KILIMANJARO KUJITATHIMINI NA KUJIPANGA UPYA

Chadema Wajichimbia Kilimanjaro Kujitathimini



Siku 74 baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kimefanya kikao cha kujitathmini na kuweka mpango kazi kwa miaka mitano ijayo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa alishindwa na Rais John Magufuli wa CCM aliyepata kura Milioni 8.8 sawa na asilimia 58.5.

Lowassa alipata kura Milioni 6 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.Chadema pia ilipata wabunge 70, wakiwamo 36 wa viti maalumu huku CCM ikipata wabunge 188. 

Katika chaguzi ndogo saba zilizofanyika baada ya uchaguzi huo mkuu, CCM iliongeza wabunge takribani tisa, wakiwamo wa viti maalumu watatu na Chadema mbunge mmoja wa kuchaguliwa.

==>Hii ni Taarifa Iliyotolewa na chama hicho jana
Katika utaratibu wake wa kujipanga na kuendelea kutekeleza mikakati na malengo ya muda mfupi na muda mrefu kwa ajili ya kufikia lengo kuu la kushinda uchaguzi, kushika dola na kuongoza serikali kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa na utamaduni wa kuwa na vikao vya kujitathmini na kufanya uchambuzi kila baada ya uchaguzi mkuu na kuweka mpango kazi unaopaswa kutekelezwa na chama kwa miaka mitano inayofuata.

Vikao vya namna hiyo pia vimekuwa vikifanyika kila mwanzoni mwa mwaka mpya, lengo kubwa likiwa ni kufanya tathmini na uchambuzi wa utekelezaji wa mpango kazi huo na kuweka mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele kwa mwaka husika kulingana na mpango huo.

Mapendekezo ya vikao hivyo vya kiuchambuzi na tathmini (retreats) huwasilishwa kwenye vikao vya kikatiba vya chama kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi kwa ajili ya utekelezaji wake kadri inavyoelekezwa na vikao husika katika ngazi mbalimbali za chama.

Ni vikao vya namna hii ambavyo huwakutanisha viongozi wa kisiasa, watendaji na wataalam wa masuala mbalimbali, vimekuwa moja ya nguzo muhimu za CHADEMA katika kujipanga na kuweka mikakati ya kukisuka na kukiimarisha chama kwa ajili ya kutekeleza lengo kuu la kushika dola kwa kuiondoa CCM madarakani na hatimaye kuwaongoza Watanzania kufikia matamanio ya MABADILIKO YA KWELI, badala ya ‘cosmetic changes’ kama inavyofanyika sasa chini ya CCM.

Katika utaratibu huo huo ambao umeshakuwa ni utamaduni wa CHADEMA kwa miaka mingi sasa, vikao hivyo vinaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa mpango kazi wa mwaka 2010-2015 na kupanga kwa ajili ya 2016-2020 na kupendekeza kwa ajili ya 2016 kabla ya kuwasilisha kwenye vikao vya maamuzi kwa mwaka huu, ambavyo vitakaa kulingana na utaratibu wa kikatiba.
 
Ufafanuzi unaotolewa kupitia taarifa hii, utasaidia kusahihisha habari ambazo hazina ukweli zinazolenga kupotosha umma, zinazoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kwa makusudi au kwa kutokujua taratibu za CHADEMA katika kupanga na kuendesha mambo yake.

Imetolewa  Alhamis, Januari 7, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

No comments:

Post a Comment