POLISI
wilayani Igunga mkoani Tabora inamshikilia mfanyabiashara kwa tuhuma za
kumjeruhi kwa bastola mwalimu wa Shule ya Msingi Saint Leo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tabora, Hamisi Selemani alisema tukio hilo ni la usiku wa Januari 15
mwaka huu katika baa ya Kibo iliyoko barabara ya Mwanzugi mjini Igunga.
Mganga
Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Igunga, Abdallah Ombeni
amethibitisha kumpokea Mwalimu Theophano Mvula akiwa na jeraha kichwani
ambapo alitibiwa kwa kushonwa nyuzi tatu na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Kamanda Selemani alimtaja mwalimu aliyepigwa risasi kuwa ni Teophano Mvula mkazi wa mtaa wa Nkokoto kata ya Igunga.
Aidha kamanda huyo alisema chanzo cha kupigwa risasi mwalimu huyo ni kujisaidia haja ndogo jirani na gari la mfanyabiashara huyo, Felix Peter Mselel (42) mkazi wa Nzega.
Alibainisha
kuwa baada ya kumuona mwalimu katika gari yake, aliamua kumfuata na
baadaye yalitokea mabishano, hali iliyofanya mfanyabiashara kuchomoa
bastola na kupiga risasi hewani huku risasi ya pili akimlenga kichwani
mwalimu huyo.
Alisema
baada ya kupigwa risasi mwalimu alianguka chini ambapo wasamaria
walimchukua na kumkimbiza katika hospitali ya wilaya ya Igunga.
Hata
hivyo, Kamanda Selemani alisema tayari mshitakiwa amekamatwa pamoja na
bastola yake ikiwa na risasi 10 ambapo anategemewa kufikishwa mahakamani
wakati wowote ili kujibu tuhuma inayomkabili.
Aidha
Kamanda Selemani ametoa mwito kwa kamati zinazojadili na kupitisha
majina ya watu wanaoomba kumiliki silaha kuwa makini, kwani bila kufanya
hivyo inasababisha kupewa silaha watu wasiokuwa na sifa za kumiliki
silaha jambo ambalo ni hatari.
Mwalimu Teophano Mvula akizungumza kutoka hospitali hapo, aliomba serikali kuwa makini na utoaji wa silaha kwa baadhi ya raia.
No comments:
Post a Comment