Saturday, January 30, 2016

CCM Yaipongeza ZEC Kutangaza Tarehe Ya Marudio Ya Uchaguzi Zanzibar .....

CCM Yaipongeza ZEC Kutangaza Tarehe Ya Marudio Ya Uchaguzi Zanzibar .....Yawataka Wananchi Kujitokeza Kwa Wingi Kupiga Kura



CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  kimeelezea kuridhishwa kwake na maamamuzi ya Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kutangaza siku ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio kwa nafasi ya Urais, Uwakilishi na Udiwani.

Kimesema  maamuzi  ya kufanyika uchaguzi huo Machi 20 mwaka huu, yanaenda sambamba na matakwa ya wananchi waliokuwa wengi katika kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa mujibu wa miongozo ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari  Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu alisema kwamba CCM inaungana na vyama vingine vya kisiasa nchini vilivyobaini kasoro za uchaguzi mkuu uliopita kuwa na kasoro na kuunga mkono maamuzi ya ZEC kuwa ni sahihi kwani yamefuata hatua muhimu za Kikatiba.

Waride alisema msimamo wa CCM katika Mkwamo wa kisiasa uliopo Zanzibar ni kurudi katika uchaguzi wa marudio ili kila chama cha kisiasa kinachoshiriki katika uchaguzi uliopita kipate haki ya kungia madarakani kwa njia halali na zinazokubalika kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo  Waride alieleza kwamba maamuzi hayo ndiyo kipimo sahihi cha kuweka uzani wa ukomavu wa kisiasa na demokrasia katika mfumo wa vyama vingi kwani lazima kila chama chenye haki ya kushiriki katika uchaguzi kiridhike na hatua zote zinazofanywa mpaka kupatikana kwa mshindi anayeongoza  kwa wingi wa kura halali.

“ Tunachukua fursa hii kuwaomba wananchi wote wenye haki ya kupiga kura hasa wafuasi wa CCM pamoja na wananchi wote wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura  Machi 20 mwaka huu.

"Tukumbuke kwamba maamuzi hayo yamefanywa na Chombo chenye Mamlaka ya kusimamia masuala yote ya Uchaguzi nchini baada ya kujiridhisha kuwa kuna kasoro zilizotokea katika uchaguzi uliofutwa na kuona kuna haja ya kila mwananchi kupata haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka kwa njia huru, wazi na zinazokubalika kisheria”. Alifafanua Waride na kuongeza kuwa uchaguzi huo ndiyo njia mwafaka ya kumaliza mkwamo wa kisiasa Zanzibar.

Katibu huyo aliongeza kwamba pia wanaunga mkono msimamo wa vyama vya vyote vya kisiasa vilivyokubali kushiriki uchaguzi wa marudio pamoja ushauri wa Msajili wa Vyama vya Sisasa nchini, Francis Mtungi kwa kuvitaka vyama vyenye usajili kushiriki katika mchakato huo ili kudumisha Demokrasia na malengo na malengo ya vyama kutumia uchaguzi kushika Dola.

Akizungumzia suala la CUF kususia Uchaguzi wa marudio alisema kwamba walichofanya ni mwendelezo wa migomo na kususa kwa mipango  ya maendeleo inayofanywa na mamlaka za serikali katika kufanya mipango mbali mbali ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi, hivyo hakuna jipya wala athari inayoweza kuathi hali ya kisiasa Zanzibar.

Alisema kwamba upinzani wa aina hiyo hauna nia njema ya kujenga maendeleo ya nchi bali una nia malengo ya kukwamisha na kudumaza maendeleo ya nchi kwa maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoweka mbele tamaa ya madaraka kuliko maisha ya wananchi.

“ Kila chama kina sera zake na misimamo yake sasa wao kama wameona kususia uchaguzi wa marudio ndiyo njia ya kumaliza mkwamo wa kisiasa Zanzibar hiyo ni juu yao,  lakini sisi tutashiriki kikamilifu ili chama chetu kipate ridhaa ya wananchi kurudi madarakani ya kidemokrasia."

Aidha alisema  chama hicho kinaamini kwamba Uchaguzi Mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka 2015 ulikuwa na kasoro nyingi zilizosababisha uchaguzi huo kukosa sifa ya kuwa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye kufutwa.

Kupitia taarifa hiyo Waride wamewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara wa mikoa minne kichama ya Unguja katika uzinduzi wa miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM itakayofanyika katika  Afisi kuu ya CCM Kisiwandui, January 31 mwaka huu.

Alisema Mgeni rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein.
Mpekuzi blog

No comments:

Post a Comment