Balozi Seif Ali Idd Akutana na Rais Magufuli leo Ikulu.....Amhakikishia Kuna Amani Zanzibar na Wanasubiri Tarehe ya Uchaguzi itangazwe
Makamu
wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali
Idd amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli kuwa hali ya Zanzibar ni shwari na Wazanzibar wanasubiri
kutangaziwa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi.
Balozi
Seif Ali Idd ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20
Januari, 2016 mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais
Magufuli.
"Mimi
nimekuja kumpa taarifa juu ya hali yetu Zanzibar inavyokwenda,
nimemueleza kwamba Zanzibar ipo salama, Zanzibar ina utulivu na ina
amani, nimeona nije nimueleze kwa kuwa yeye ni kiongozi wetu" alisisitiza Balozi Seif Ali Idd.
Makamu
huyo wa pili wa Zanzibar ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa amani na
utulivu, wananchi wa Zanzibar wanaendelea na shughuli zao kama kawaida
tofauti na inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
"Hayo
yanayoandikwa kwenye magazeti kuwa Zanzibar kuna fujo, Zanzibar
kutatokea machafuko sio kweli, na kama unavyojua uchaguzi ulifutwa na
tume ya uchaguzi na tunasubiri tarehe mpya ya uchaguzi itangazwe na tume
ili tufanye uchaguzi" amebainisha Balozi Seif Ali Idd.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment