Jukwaa La Wahariri, Saed Kubenea Watoa Onyo Kwa Nape Nnauye Kwa Kulifungia Gazeti La Mawio
MKURUGENZI
wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea pamoja na Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Absalom Kibanda wameionya serikali
juu ya uamuzi wa kulifuta gazeti la MAWIO uliochukuliwa hivi karibuni.
Kupitia
tangazo la serikali lenye notisi namba 55, serikali ilichukua uamuzi wa
kulifungia MAWIO, Januari 15, 2016 huku Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akisema gazeti hilo limekuwa ‘sugu’ kwa
uchochezi tangu 2013.
Kubenea
na Kibanda walikuwa katika kituo cha Polisi cha Kati ambapo ndiyo Makao
Makuu ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakiwasindikiza wahariri Jabir
Idrissa na Simon Mkina walioitikia wito wa uliotolewa na jeshi hilo siku
tatu zilizopita.
Kibanda
amewambia wanahabari kuwa kitendo cha jeshi la polisi kuwasaka ili
kuwakamata Jabir na Mkina ambao ni wahariri ili kuwahoji huku gazeti la
MAWIO likiwa limefungiwa, kinalenga kuwatisha waandishi wa habari nchini
na kuzima uhuru wa habari.
Ameulezea
uamuzi huo wa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Habari, Nape, kama
uamuzi uliolishitua TEF na wamewasiliana naye wakielezea mshituko na
masikitiko yao.
“Hatuwezi
kuvumilia kufungiwa kwa vyombo vya habari, kukamatwa na kunyanyaswa kwa
waandishi, miaka miwili iliyopita nilitakiwa kujisalimisha makao makuu
ya polisi, nikafikishwa mahakamani na nikashinda kesi, naelewa maumivu
ya mapambano haya,” ameeleza Kibanda.
Kwa
upande wake Kubenea, amesema Serikali kupitia Nape imechukua uamuzi wa
kikatili dhidi ya gazeti la MAWIO ili kuzima sauti ya wananchi kwa hoja
zisizo na mashiko ikiwemo ile ya uchochezi ambayo imekuwa kisingizio cha
watawala kwa muda mrefu.
“Katika
toleo la MAWIO lilimnukuu Maalim Seif akijitangaza mshindi, yeye
hakuitwa mchochezi, Jecha amefuta uchaguzi wakati hana mamlaka ya
kisheria wala ya kikatiba hakuitwa mchochezi ila gazeti kuandika ushindi
uliotangazwa na Seif limefungiwa,” ameeleza Kubenea.
Kubenea
ameongeza kuwa, ubovu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 umekuwa
ukitumiwa na serikali kuviadhibu vyombo vya habari vinavyofichua maovu,
huku mahakama ikithibitisha mara kadhaa kuwa madai ya uchochezi
yanayotolewa na serikali hayana mashiko.
“Jabir
ni Mwandishi aliyebobea kitaaluma na uzoefu, ameandikia magazeti ya
Uhuru, Mzalendo, Majira na New Habari huko kote hakuitwa mchochezi wala
hakukamatwa.
“Nape
alikuwa mmoja wa waandishi na vyanzo vya taarifa za MwanaHALISI kipindi
hana madaraka CCM, mbona alishirikiana na sisi kuibua maovu kama sisi
ni wachochezi?” alihoji Kubenea.
Jabir
na Mkina wamekuwa wakitafutwa na jeshi la polisi kwa siku tatu
mfululizo tangu Jumamosi kwa tuhuma za uchochezi huku jaribio la
kuwakamata likishindikana mara kwa mara kutokana na kutojua walipo mpaka
walipoamua kujisalimisha jana.
Mbali
ya Kubenea na Kibanda, walisindikizwa pia na Mhariri Mtendaji wa gazeti
la MwanaHALISI, Ansbert Ngurumo pamoja na wakili wao, Fredrick Kihwelo.
No comments:
Post a Comment