Wabunge wa CCM Wapeana Mikakati ya Kuwakabili Wabunge wa UKAWA.......Wamgeuka Rais Magufuli Kuhusu Bomoabomoa na Kuwabana Wafanyabiashara
Wabunge
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamemgeuka Rais Dk. John Magufuli na
kutaka kasi yake iangaliwe upya vinginevyo inaweza kukigharimu chama
hicho tawala kwa wananchi.
Tangu
Rais Magufuli aingie madarakani kumekuwa na hatua mbalimbali
zilizochukuliwa ikiwamo kuifumua Bandari ya Dar es Salaam na kusimamisha
vigogo kadhaa pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru), Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahaco) na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA).
Hatua
nyingine ni kubomoa nyumba katika bonde la Msimbazi na Mkwajuni jijini
Dar es Salaam na kuwafukuza wafanyakazi wageni wasio na vibali.
Wakizungumza
katika vikao vya siri vilivyoanza mjini Dodoma tangu juzi na
kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, baadhi ya
wabunge wanaelezwa kuonyesha hofu ya hatua hizo kuwa huenda
zitakigharimu chama chao kwa wananchi.
Wabunge
hao wapo mjini Dodoma kwa ajili ya semina ya siku mbili yenye lengo la
kupata mbinu za kupambana na kambi ya upinzani ambayo imefanikiwa
kuongeza idadi ya wabunge katika Bunge la 11 litakaloanza rasmi wiki
ijayo.
Taarifa
kutoka chanzo cha uhakika ndani ya vikao hivyo, zilisema kuwa wabunge
hao walilalamikia suala la bomoabomoa kwamba linakichafua chama chao
mbele ya wananchi na kuhoji kama hakukuwa na njia nyingine za
kuwahamisha wananchi hao.
“Wabunge
wametaka ubomoaji usitishwe kwa waliojenga ndani ya mita 60, ila
afadhali ufanywe kwa walio mabondeni kabisa. Wengine walishauri kuwa
ubomoaji ungeachwa kabisa hadi mvua zianze ndipo wawaondoe,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo
chetu kilisema kutokana na hoja za wabunge hao, ilimlazimu Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kulazimika kusimama
na kuanza kutetea suala la bomoabomoa na kusema kuwa hatua hiyo
ilichukuliwa ili kuwanusuru wananchi na mafuriko wakati wa masika.
“Hata
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju naye alisisitiza kuwa
Serikali inafuata sheria katika ubomoaji huo, huku akiwatoa hofu kwamba
uamuzi huo hautakiathiri chama,” kilisema chanzo chetu ndani ya vikao hivyo.
Mbali
na bomoabomoa ambayo inaendelea, masuala mengine yaliyoibuka katika
semina hiyo ni pamoja na kuwabana wawekezaji na wafanyabiashara kiasi
cha kuwabughudhi.
“Wabunge
wameitaka Serikali isiwajengee hofu wafanyabiashara na wawekezaji
katika kulipa kodi, bali watazamwe ili wasione mazingira magumu ya
kufanya biashara,” kilisema chanzo.
Kutokana
na hali hiyo, wabunge walimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip
Mpango kukutana na wafanyabiashara na sekta binafsi ili kuwarudishia
imani.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli alikutana na wawakilishi wa sekta binafsi jijini Dar es Salaam.
Suala
jingine lililojadiliwa kwenye vikao hivyo ni la kuwaruhusu wabunge wa
kuteuliwa kuingia kwenye uchaguzi wa mameya, hasa kwa Jiji la Dar es
Salaam ambalo Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa, George Simbachawene alilitolea ufafanuzi.
Akizungumza
na wabunge hao, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, aliwataka kutobweteka na
kuitetea Serikali bali waibane na kuondoa sheria kandamizi za kikoloni.
“Kinana
amewaambia wabunge wa CCM wasipokuwa wakali katika kuibana Serikali
watakiponza chama na kukifanya kianguke. Kinana ametuagiza tupambane
kuondoa sheria kandamizi ikiwamo kupunguza kodi ya mafuta.
“Amesema tabia ya kuwaachia wapinzani ndio waibane Serikali iachwe na badala yake kila mtu awe mwiba,” kilisema chanzo.
Pamoja
na hali hiyo wabunge hao pia walijadili hatima ya vyombo vya habari
nchini ambapo walitaka wamiliki wa vyombo hivyo kuwalipa mishahara
mizuri waandishi wa habari na vikishindwa vijiondoe vyenyewe kwenye
biashara hiyo.
Wametaka
pia Serikali itunge sheria itakayoweka viwango vya elimu kwa waandishi
wa habari ili kuondoa usumbufu kwa waandishi wasio na sifa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Bara, Pius Msekwa, aliyetoa mada ya ‘Wajibu wa mbunge wa CCM katika mfumo wa vyama vingi’ alieleza jinsi kambi ya upinzani bungeni inavyokuwa na mkakati wa kuidhoofisha Serikali ili katika uchaguzi wachukue madaraka.
Aliwataka wabunge wa CCM kutafuta mbinu madhubuti za kujilinda na kujitetea ili kuzuia hilo lisitokee.
Alisema
ni wajibu wa kila mbunge wa CCM kuiwezesha Serikali ya chama chake
kutekeleza majukumu yaliyoahidiwa katika ilani ya uchaguzi kwa kupitisha
miswada ya sheria inayowasilishwa na Serikali kwa madhumuni hayo
ikiwamo bajeti zinazopendekezwa.
“Kwahiyo
ni halali kabisa kwa wabunge wa CCM kutumia uwingi wao kuidhinisha
maombi ya bajeti yanayoletwa bungeni na Serikali ili kuiwezesha nayo
itimize ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya
chama,” ilisema sehemu ya mada ya Msekwa.
Alipoulizwa
na waandishi wa habari kuhusu vikao hivyo, Katibu wa wabunge wa CCM
ambaye pia ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Ajira na Vijana, Jenister Mhagama, alisema hivyo vilikuwa vikao
vya chama hivyo anayepaswa kuzungumzia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye.
Naye Nape alipoulizwa kuhusu vikao hivyo, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa ni vya siri.
M
No comments:
Post a Comment