Thursday, January 21, 2016

Ndalichako afuta mfumo wa GPA

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako Aufuta Mfumo wa GPA Na Kurudisha Mfumo wa Divisheni kwa Kidato cha Nne Na Sita


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amefuta mfumo wa matokeo ya GPA kwa wanafunzi wa kidato cha nne, sita na ualimu na kurudisha ule wa zamani wa divisheni.

Mbali na hilo, Ndalichako ameagiza kuondolewa kwa mtihani wa pili (paper two) kwa watahiniwa binafsi ambao ulianza mwaka 2014.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Profesa Ndalichako alisema Serikali haitawavumilia watu ambao wanataka kuchezea elimu.

“Nilitembelea Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Januari 7, nikaagiza wanipe sababu za msingi za kutoka divisheni kuingia GPA, hadi leo wameleta maelezo bila ya sababu za msingi na maelezo yao yamejikita katika blabla ambazo hazijitoshelezi,” alisema Profesa Ndalichako ambaye katika mkutano huo aliongozana na naibu wake, Stella Manyanya na Katibu Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde.

Alisema kuna mgongano mkubwa katika upangaji wa GPA kwani kidato cha nne ufaulu unaanzia 3.6 -5, kidato cha sita katika daraja hilo wanaanzia 3.7 -5 wakati ufaulu kama huo kwa mafunzo ya ualimu unaanzia 4.4 -5 ambao ni mkanganyiko mkubwa unaozalisha watu wasio na ubora wa kiwango husika.

“Baadhi ya watahiniwa waliopitia katika mfumo huo na kufaulu wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu,” alisema.

Alisema kuwapo gredi E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA, kunawafanya watahiniwa waliopata E kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote ambao wanahesabiwa wamefaulu.

Alisema Necta imetoa maelezo mengi ambayo yameonekana hayana uhalisia wala wa kukamilisha sababu badala yake wamejikita katika visingizio.

Alisema Necta walimweleza kuingia katika mfumo huo ilikuwa ni maoni ya wadau lakini alipowauliza ni wadau kiasi gani na mikutano hiyo ilifanyikia wapi, hawakuwa na majibu na hakuna hata mkutano ambao uliwahi kufanyika.

“Jambo jingine lazima mkumbuke kuwa, mfumo huu haujaenda hata kwa kamishna wa elimu kupata kibali, ndiyo maana wadau waliniambia kuwa nisingetoa siku saba badala yake ningeufuta mara moja,” alisema Ndalichako.

Alipinga madai kwamba uliruhusiwa na Serikali, akisema ulianza kutumika tangu 2014 wakati maagizo ya Serikali Mtandao (EG) yalieleza kuwa kila kitu kianze kutumika Juni 16, mwaka huu.

Alisema alidanganywa kwa kuambiwa wizara iliagiza wakati amebaini kuwa wizara ilipitisha kanuni za mitihani Oktoba 28, 2015 na kuingiza katika gazeti la Serikali Novemba 6 mwaka jana ikiwa ni miaka miwili tangu mfumo wa GPA uanze kutumika.

Kwa upande wa watahiniwa binafsi, alisema kuanzia sasa hakutakuwa na mitihani miwili ambayo mmoja ulikuwa ni kwa ajili ya upimaji endelevu, hivyo watahiniwa watafanya mtihani mmoja tu.

Hata hivyo, Dk Msonde alisema watahiniwa binafsi wa sasa watasahihishiwa mitihani yao kwa mfumo wa mitihani miwili kwa kuwa walishafanya.

No comments:

Post a Comment