Saturday, January 2, 2016

"SERIKALI YA MAGUFURI NI KUBWA WALA HAIBANI MATUMIZI" ASEMA DR.MAKONGORO MAHANGA

Dk Makongoro Mahanga Amvaa Rais Magufuli Kwa Kuunda Serikali Kubwa Tofauti Na Ahadi Yake Aliyoitoa wakati wa Kampeni


Wakati watu mbalimbali wakimminia sifa Rais John Magufuli kwa kubana matumizi, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga amesema uwingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya yake ya kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri.

Dk Mahanga alikuwa Naibu Waziri wa Lazi na Ajira tangu mwaka 2008 na hakuwahi kuhamishwa wala kupandishwa hadi ngazi ya uwaziri hadi Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilipomaliza muda wake na baadaye kujiunga na Chadema.

Katika waraka wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Dk Mahanga alimkosoa Rais Magufuli akisema ameongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri baada ya kuteua makatibu wakuu 27 wakati anawaaminisha wananchi kwamba wizara ni 15 tu.

Dk Magufuli ameunda baraza lenye mawaziri 15, na manaibu waziri 19 na hivyo kufanya baraza lake kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 55. 
Uamuzi wa kupunguza idadi ya wizara ulikumbana na changamoto ya nafasi za makatibu, ambao hata hivyo baadhi amewarudisha wizarani ambako watapangiwa kazi na kubakiwa na makatibu 27.

“Si kweli kwamba kapunguza ukubwa wa Serikali, bali kaongeza ukubwa wake. Sina hakika kama wasaidizi wa Rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema Dk Mahanga akifafanua kuwa katibu mkuu ndiye mtendaji mkuu wa wizara na afisa masuhuli.

Alisema katibu mkuu ndiye mwenye dhamana ya utendaji na ndiyo maana hata katika ngazi ya kata, ofisi inaitwa ofisi ya ofisa mtendaji wa kata na si ofisi ya diwani.

Kwa maana hiyo, Dk Mahanga, ambaye kitaaluma ni mhasibu, alisema Rais alipounda Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambazo awali zilikuwa mbili tofauti na kuteua makatibu wakuu watatu, kiuhalisia hakuunganisha wizara mbili kuwa moja bali ameunda wizara tatu kutoka mbili za awali.

“Ongezeko la gharama kwa kuongeza waziri mmoja ni ndogo sana kulinganisha na kuongeza katibu mkuu mmoja. Waziri anapoteuliwa tayari anakuwa ni mbunge mwenye mshahara wake wa ubunge na kinachoongezeka ni kama laki tano tu juu ya ule mshahara wa ubunge na gharama nyingine ndogo za gari, pia mishahara na gharama za katibu muhtasi, msaidizi na dereva,” alisema Dk Mahanga.

Alisema kwa ujumla ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni kwamba ataunda Serikali ndogo, hakuitimiza badala yake ameongeza ukubwa wa Serikali.

Wakati wa kampeni na alipoapishwa, Rais Magufuli alisema ataunda baraza dogo la mawaziri, hiyo ilijenga shauku kwa wananchi kufahamu kiwango cha ukubwa au udogo wa baraza hilo ikilinganishwa na mabaraza yaliyoundwa na watangulizi wake, tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.

Dk Magufuli pia alitoa ahadi hiyo alipozindua Bunge Novemba mwaka jana mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment