Luqman
Maloto ameandika makala hii yenye picha ya utajiri mkubwa wa mbunge wa
Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa rais wa awamu ya nne, Jakaya
Kikwete.
Makali
hii inayomhusu ‘Ridhiwani’ itakuvuta na kukumbusha hadithi moja iliyowahi
kuandikwa katika kitabu chenye riwaya ya ‘lugha gongana’ ya sikuelewi.
‘Sikuelewi’ ilipata umaarufu mkubwa miaka ya 1990’s.
Endelea
hapa na makala ya Luqman:
Ukipanda
daladala huwa hakuna mfumo unaoeleweka, siku nyingine utakutana na kelele kama
sokoni, wale wanaongea yao, hawa wanabishana hivi, hapa napo kuna ubishi wa
soka.
Siku
nyingine ndani ya daladala kama mnasindikiza msiba, kimya kinatawala. Wakati
mwingine kuanzia mwanzo wa kitu mpaka mwisho ni ugomvi tu kati ya kondakta na
abiria. Kimsingi daladala huwa haina utaratibu maalum.
Nikipanda
daladala huwa napenda kukaa siti ya mbele au karibu na dereva ili nijifunze
jinsi ya kuendesha. Si unajua tena, wanasema ukiwa karibu na mahakama lazima
utajua vifungu vya sheria. Matunda ya ujirani hayo.
Nikiwa
namtolea macho dereva jinsi anavyobadili gia kwa mbwembwe, abiria aliyekuwa
amekaa pembeni yangu akanifinya, nilipogeuka akanipa ishara nitazame mlangoni.
Kulikuwa na mrembo anaingia.
Yule
abiria jirani yangu alimfuatilia yule mrembo mpaka alipokwenda kuketi, kisha
akanigeukia na kuniambia: “Kama umeona mambo ya Ridhiwani Kikwete?”
Nikawa
sijamuelewa, nikamuuliza: “Ridhiwani Kikwete amefanya nini hapo?”
Akasema:
“Kaka si unaona mwenyewe mwanamke alivyo mzuri, ameumbika. Yule siyo wa
kawaida.”
Nikamuuliza
tena: “Sasa kuumbika kwa huyo mwanamke kunahusiana nini na Ridhiwani?”
Akanijibu:
“Kumbe wewe ndugu yangu umechelewa mjini, nilivyokuona nilidhani mchangamfu
mwenzangu wa jiji. Kwa taarifa yako misemo yetu sisi watoto wa mjini ni kwamba
vitu vizuri tunaita mambo ya Ridhiwani.
“Magari
yote mazuri mjini ni Ridhiwani, vituo vya mafuta vikubwa vyote Ridhiwani,
maghorofa makubwa ni Ridhiwani, ndiyo maana na wanawake wazuri wote mjini tunasema
ni mambo ya Ridhiwani.”
Aliposema
hivyo, alinikumbusha kitu. Ikabidi niingie kazini kufanya mahojiano, maana
habari za Ridhiwani na utajiri wake ni nzito na zimekuwa zikizungumzwa kwa
kitambo kirefu sasa.
Nikamuuliza
yule abiria: “Lakini ndugu yangu wewe si una mke? Ni mzuri au mbaya?”
Akajibu:
“Wewe unaniona mimi wa kuja? Siwezi kuoa mwanamke mbaya. Mke wangu chuma, kisu
kikali, mrembo hasa, tena niliwahi kugombana na Hashim Lundenga alipotaka
kumchukua kumuingiza kwenye mashindano ya Miss Tanzania.”
Hapahapo
ndipo nilikuwa napataka, nikamuuliza: “Wewe mkeo akiitwa wa Ridhiwani
utafurahi?”
Haraka
sana alijibu: “Thubutu, patachimbika siku hiyo.”
Uzuri
alikuwa anajileta mwenyewe, nikampiga swali lingine: “Sasa mbona wewe unaona
sawa kusema wake wa wenzako kuwa ni mali ya Ridhiwani?”
Safari
hii kwa utulivu akasema: “Umeniuliza swali lenye maana kubwa, unajua mjini watu
wanakuza sana maneno. Kuna kipindi nilikuwa nikisikia jina la Ridhiwani
nilikuwa naogopa, siku nilipomuona nikashangaa, kumbe mtu mwenyewe ana umbo
dogo tu, tena wa kawaida.”
Aliposema
hivyo, siti ya nyuma yetu alikuwepo mtu ambaye alikuwa anafuatilia mazungumzo
yetu, akauliza: “Samahani kaka, kama sijakosea nimekusikia ukisema Ridhiwani
ana umbo la kawaida, tena dogodogo, hivi ni kweli?”
Abiria
pembeni yangu akajibu: “Wa kawaida ndiyo, kwani ulifikiriaje?”
Abiria
wa siti ya nyuma akasema: “Jamani hii dunia kumbe unaweza kumuogopa mtu mdogo
ambaye unaweza hata kumzaa. Mwenzenu kwa jinsi stori za Ridhiwani zilivyo na
jinsi anavyozungumzwa, mimi nilifikiri ni jitu kubwa la miraba minne mara 10.
“Tena
niseme ukweli, mimi nilikuwa nafikiri Ridhiwani ni mkubwa kama zimwi, yale
madude ya kutisha ya kwenye hadithi za kale. Nashangaa leo unaniambia kumbe Ridhiwani
wa kawaida tu. Kusema ule ukweli leo nimestaajabu.”
Abiria
mwingine naye akachangia, sasa mada ilikuwa imeshakua na kupanuka ndani ya
daladala. Huyu alikuwa mzee. alisema: “Nyie vijana, mimi mwenyewe nilikuwa
nasikia sana habari za Ridhiwani kuwa anamiliki mali nyingi, na nikawa naamini
kweli na nikawa natangaza.
“Juzi
hapa nikashangaa kuna nyumba yangu ghorofa moja nilijenga wakati mambo yangu
yakiwa mazuri, nimeshindwa kuimaliza kwa sababu fedha zimekata, ghafla nakuta
watu wanaijadili kuwa ile nyumba yangu ni ya Ridhiwani ameisahau ndiyo maana
hajaimaliza.
“Tena
wale watu walikuwa wanasema Ridhiwani ana nyumba nyingi mpaka nyingine
anazisahau. Niliwaambia ile nyumba ni yangu, hakuna aliyenielewa, tena
waliniambia nimetumwa.”
Sauti ya
kike kutoka nyuma ikasikika: “Kila kitu wanasema cha Ridhiwani, magari,
majumba, makontena, migodi, bado kidogo wataanza kutangaza na wake zao ni mali
ya Ridhiwani. Ikifika kipindi hicho tukumbushane.”
Mwanamke
mwingine akadakia: “Bado kidogo wapi? Mwenzenu usiku leo nimepokea mkong’oto wa
maana kutoka kwa mume wangu, kanipiga kweli. Hatukuwa na ugomvi wowote, kafika
ananiuliza kama namfahamu Ridhiwani, nikamjibu ndiyo. Hapo ndiyo ikawa chanzo
cha ugomvi.
“Akaniuliza
tena namfahamu kivipi, nikamjibu kupitia kumsoma kwenye magazeti na kumuona
katika televisheni. Mume wangu hakuamini, akasema hana imani na mimi kwa sababu
anasikia wanawake wote wazuri ni wa Ridhiwani. Nikamwambia aache wivu wa
kijinga, hapo ndipo nilianza kupokea mkong’oto. Mwili wote unauma hapa nilipo.”
Gari
lilikuwa limefika Posta, nilipokuwa nashuka nikapata wazo la kuendelea na
usaili wangu. Nikamuuliza mpigadebe mmoja: “Unamfahamu Ridhiwani Kikwete?”
Akanijibu:
“Namfahamu sana Ridhiwani, yule ni kibosile. Kwanza ni mwili nyumba, bajeti ya
serikali yote inamtegemea yeye. Hapahapa mjini ana majumba kibao.”
Mpigadebe
akaanza kunionyesha nyumba za Ridhiwani, akasema: “Unaona hii hapa? Mwenyewe ni
Ridhiwani. Ila unajua Ridhiwani huwa hapendi sifa za kujulikana kama ana
utajiri mkubwa, ndiyo maana hii hapa imeandikwa Benjamin William Mkapa Pension
Tower. Huyu Benjamin amewekwa kama geresha tu. Mwenye mali Ridhiwani.”
Akanizungusha,
akasema: “Unaona hii?” Ni jengo la PPF Tower, akasema: “Huyu PPF Tower naye
amewekwa tu kama geresha, hili ghorofa la Ridhiwani.”
Tukasogea
mbele, tukakutana na jengo la Golden Jubilee Tower, akasema: “Kama umeona
Ridhiwani alivyo mjanja, yaani majengo yake yote ameyapa majina tofauti. Huyu
Golden Jubilee Tower naye kawekwa tu hapa, mwenye mali ni Ridhiwani.”
Tukiwa
tumesimama nje ya jengo la Golden Jubilee, mpigadebe akanionesha jengo la Viva
Tower, akasema: “Lile pia la Ridhiwani. Viva Tower naye kama wenzake, amewekwa
tu. Nimeshakwambia Ridhiwani hapendi sifa.”
Tukiwa
tunatembea kwa miguu kunionesha mali za Ridhiwani ambazo mpigadebe huyo
anazijua, alisema: “Ila ukitaka kujua kama Ridhiwani ni mjanja, majengo yake
yote jina la mwisho ameita tower ili wasimuibie. Tower ni jina la mtoto wake.”
Tukajikuta
tumesimama nje ya majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), mpigadebe
akaniambia: “Kama nimekwambia kuna watu wana fedha hapa nchini, unaona haya
maghorofa mawili mbele yetu yanayofanana? Yote haya ni ya Ridhiwani.”
Hapo
nikaguna, nikamuuliza: “Mbona haya majengo ni ya BOT?”
Naye
akaniuliza: “BOT ndiyo nini?”
Nikamjibu:
“BOT maana yake ni Benki Kuu.”
Huku
akitabasamu, akasema: “Unaona sasa, bila shaka utakuwa umeamini haya majengo ni
ya Ridhiwani kwa sababu hata hiyo Benki Kuu unayoisema ni ya Ridhiwani.”
Mpigadebe
akanipeleka kwenye majengo pacha marefu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati,
PSPF Commercial Twin Tower, tukaenda Rita Tower, Uhuru Heights, Umoja wa Vijana
Complex na mengine mengi, kote huko alisema: “Mambo ya Ridhiwani kaka, huyu mtu
ni kiboko.”
Kwa
kutumia simu yangu, ‘niligugo’ na kupata picha ya Ridhwani, nikamuonesha yule
mpigadebe kisha nikamuuliza kama anamfahamu, akanijibu ni sura ngeni, hamtambui
kabisa.
Nikamwambia
huyo ndiye Ridhiwani, yule mpigadebe nusura anichape makofi, akasema: “Toa
ujinga wewe, huyo mtoto mdogo anawezaje kuwa Ridhiwani? Ridhiwani ni jitu lenye
mwili wake, kwanza haonekani hovyohovyo.”
Alipoona
nimekaa kimya, akaniambia: “Huyu alikuwa rais wetu, Jakaya Kikwete si unamjua?”
Nikamjibu ndiyo, akasema: “Kwa taarifa yako Ridhiwani ndiye baba wa Kikwete,
ndiye amemfanya Kikwete awe rais, ana hela Ridhiwani mpaka mpaka yeye mwenyewe
zinampa homa.”
Nilipoachana
na yule mpigadebe, moja kwa moja nilikwenda Kariakoo, nikakutana na mtu
amejiinamia, nilipomuuliza kama anamfahamu Ridhiwani, akanijibu harakaharaka:
“Umenitajia hilo jina nahisi kama nakaribia kuuaga umaskini.”
Nikamuuliza:
“Kivipi?”
Jawabu
lake lilikuwa hili: “Natamani kukutana naye anipe kazi, si unajua anamiliki
miradi mingi? Hesabu Daraja la Kigamboni, Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, ana
mabasi na malori mpaka idadi haitambui, majumba na viwanja. Jumlisha Uwanja wa
Taifa na ule wa Uhuru baada ya kuununua, sasa hivi yupo anaufanyia marekebisho
ili uwe wa kisasa.”
Nilimaliza
usaili wangu nikiwa nimechoka kabisa. Niliporudi nyumbani jioni, nilimuuliza
mtoto wangu, Captain Nyambo: “Captain unamjua Ridhiwani?”
Captain
Nyambo alijibu: “Unamzungumzia Ridhiwani mbunge wa Chalinze, mtoto wa Dk.
Jakaya Kikwete?”
Sikuona
sababu ya kumjibu swali lake, maana aliniuliza kwa mtindo wa majigambo kuwa
anamfahamu sana, nikamuuliza lingine: “Vipi kuhusu utajiri wa Ridhiwani?”
Akanijibu
kwa kuniuliza: “Ukitaka stori za Ridhiwani kama changamsha genge, unaweza
ukashangaa hata mimi mtoto wako mpendwa naambiwa ni wa Ridhiwani, kwa sababu
kila kitu kizuri kimekuwa cha Anko Rizi.”
Nikamwangalia
Captain Nyambo, mwenyewe wala hakutetereka, akasema: “Captain Mkuu si mwenyewe
huwa unaona mambo yangu ya shuleni? Wabongo hawashindwi kusema Captain Nyambo
ana akili sana, atakuwa mtoto wa Ridhiwani.”
Alipoona
sifurahishwi na maneno yake, Captain Nyambo aliniambia: “Wewe ndiye baba yangu,
Ridhiwani hana ubavu wa kunipata, Mungu amenifanya wewe ndiye uwe baba yangu,
ndiyo maana nakupenda halafu tunaelewana sana.”
“Captain
Mkuu eeeh,” Captain Nyambo aliniita, nilipoitika alisema: “Tuache hizo stori za
Ridhiwani, hazina tija kwetu. Ila kiukweli baba Tanzania ni ya ajabu sana,
yaani kama kila kinachosemwa ni cha Ridhiwani kingekuwa kweli, basi huyu mtu
angekuwa tajiri kuliko tajiri namba moja ulimwenguni, Bill Gates.”
By Luqman Maloto
+255 713 355 717
+255 713 355 717
No comments:
Post a Comment