Ndugu wadau najua wengi wenu sio wageni na jina hili la zitto kabwe. zitto ambaye kwa sasa ni mbunge wa kigoma mjini kupitia tiketi ya ACT-WAZALENDO amekua midomoni mwa watu wengi sana katika nchi hii. Hivi karibuni kutokana na ushindani mkubwa wa kisiasa kumekua na maneno mengi yakizungumzwa juu ya wanasiasa mbalimbali . Ningependa kuchukua nafasi hii leo kumuangazia mbunge huyu maarufu miongoni mwa vijana wengi kwa kuangalia utendaji kazi wake katika medani hii ya siasa.
1. MABADILIKO
SEKTA YA MADINI
Zitto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa
mbunge mwaka 2005 akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini ambalo halina mgodi
hata mmoja wa madini ukiachana na wachimbaji wadogo wa udongo wa Pemba ambao
una soko kubwa hapa Kariakoo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo ajenda
inayomtambulisha Zitto Kabwe kwa Taifa ni ajenda ya mabadiliko makubwa
aliyoanzisha katika sekta ya Madini nyakati ambayo hakuna mwanasiasa
aliyethubutu kukosoa sera za uwekezaji kwa namna aliyofanya. Baada ya kudokezwa
kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Bwana Nazir Karamagi amesaini
mkataba mpya wa Madini akiwa hotelini nchini Uingereza, Zitto alimtaka Waziri
kujieleza ndani ya Bunge kuhusu mkataba huo na masharti yake ya kikodi. Waziri
huyo aliposhindwa Zitto aliwasilisha Hoja Binafsi Bungeni (akiwa mbunge wa
kwanza kufanya hivyo katika Bunge la Tisa na la Nane kwa pamoja). Hoja ya
Buzwagi ilisababisha Zitto kusimamishwa ubunge kwa miezi 4. Hata hivyo mnamo
Septemba 10, 2007 alitangaza Azimio la Songea lililomshinikiza Rais Jakaya
Kikwete kuunda Kamati ya Bomani ili kupitia mikataba yote ya Madini nchini.
Kutokana na kazi yake hiyo leo Tanzania ina
Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ambayo imeboresha nafasi ya
Tanzania kufaidika na Madini, imeruhusu kisheria Serikali kuwa na hisa kwenye
migodi ( na hivi tunavyoongea, kwa mfano, sasa Serikali inamiliki 50% ya Mgodi
wa TanzaniteOne). Makampuni ya Madini ambayo yalikuwa yanatangaza hasara kila
mwaka leo yanalipa kodi ya Mapato na Halmashauri zenye migodi zinalipwa ushuru
wa huduma wa mabilioni ya fedha. Huyu ndiyo Kiongozi wetu wa ACT Wazalendo.
Hawa ndio Viongozi Taifa hili linawataka. Viongozi wanaotenda na kutoa majawabu
ya changamoto za nchi. Sio Viongozi wanaolaumu tu eti wakisubiri kushika dola
ndio watende. Nani anayebisha rekodi hii?
2. KUZUIA
UBINAFSISHAJI WA SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA (NIC)
Zitto Kabwe alikuwa Waziri Kivuli wa
Mipango na Uchumi mwaka 2006 wakati Shirika la Bima la Taifa likiwa kwenye
mchakato wa Ubinafsishaji. Wafanyakazi wa TUICO Tawi la Bima walimfuata
wakielezea kwa ushahidi namna mali za Shirika zilivyopangwa kuuzwa na wajanja
wachache kutaka kujiuzia Shirika na Mali zake hasa jengo la kitega uchumi kwa
bei ya kutupwa. Zitto aliwakilisha hoja hiyo kwenye Kamati ya Bunge ya Fedha na
Uchumi chini ya Mwenyekiti wake Ndugu Abdallah Kigoda na kuishawishi Kamati
kukataa ubinafsishaji wa NIC na badala yake kuunda kikosi kazi cha kurekebisha
Shirika na liendelee kuwa Mali ya Umma.
Mwezi Novemba Mwaka 2006 Baraza la Mawaziri
lilikubaliana na hoja za Zitto alizotoa kwenye Kamati ya Bunge na ndani ya
Bunge na kuamua kuliondoa Shirika kwenye mchakato wa ubinafsishaji na leo hii
Shirika limebaki kuwa la Umma na limeanza kurudi kwenye hali yake. Aliendelea
kulisaidia Shirika la Bima kwa kuagiza (akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali ) kuwa Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma yaweke Bima
kupitia Shirika la Bima la Taifa na agizo hilo kutekelezwa na Mashirika mengi
ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania.
Sio Bima tu, Zitto akiwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma aliagiza kuondolewa katika
orodha ya ubinafsishaji Shirika la STAMICO ili liweze kushiriki kikamilifu katika
sekta ya Madini na liliondolewa. Huo ndio Ujamaa wa kidemokrasia ambao Chama
chetu cha ACT-Wazalendo kinautangaza, na huyo ndio Kiongozi wetu ambaye ana
uzalendo wa dhati kwa mali za Watanzania. Nani anayebisha rekodi hii?
3. SHERIA
YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA
Mwaka 2008/2009 Zitto Kabwe aliweka rekodi
nyingine ya kuwa Mbunge wa kwanza kuzungumzia mabadiliko ya sheria ya viongozi
wa umma ili kuipa meno secretariat ya maadili ya viongozi na kutengenisha
biashara na siasa. Alipeleka Bungeni Muswada Binafsi wa Sheria ili kufanya
mabadiliko makubwa ya Sheria Maadili. Hata hivyo muswada ule ulizuiwa na
Serikali kuingia Bungeni licha ya kukamilisha kila hatua iliyopaswa.
Leo hii Chama chetu kinazungumzia kurejesha
Miiko ya Viongozi kuna watu wanadhani Zitto kaanza haya hivi sasa, la hasha.
Huu ni mwendelezo wa yale aliyokuwa anaamini miaka kadhaa iliyopita na kwa kuwa
yeye anapenda kutembea anayoyasema alitushawishi wenzake kufanya Miiko ya
Viongozi kuwa sehemu ya Katiba ya Chama chetu. Yeye ni Kiongozi wa kwanza wa
kisiasa kuweka hadharani Mali na Madeni yake hapa nchini. ACT Wazalendo ni
chama pekee cha siasa hapa nchini ambacho Viongozi wake wanatakiwa kikatiba
kutangaza Mali zao, Madeni yao na Maslahi yao ya kibishara. Nani anabisha
rekodi hii?
4. UKAGUZI
WA MAHESABU WA VYAMA VYA SIASA
Katika kuhakikisha kuwa kila senti ya fedha
ya umma inakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, Ndugu
Zitto Kabwe aliwasilisha Bungeni mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa,
Sheria namba 5 ya Mwaka 1992 na kuwezesha CAG kukagua fedha za vyama ambazo
zinatoka Serikalini kama ruzuku. Sheria ya Vyama vya siasa inataka kila Mwaka
Serikali kutenga kiwango kisichozidi asilimia mbili (2%) ya Bajeti ya Serikali
kama ruzuku kwa vyama vya siasa. Vyama hupewa wastani wa Shilingi bilioni 20
kila mwaka na kugawana miongoni mwao lakini fedha hizi zilikuwa hazikaguliwi
kinyume na Sheria za Fedha.
Baada ya Sheria hiyo kupitishwa na Bunge
mwaka 2009, Zitto alisimama kidete kuhakikisha inatekelezwa jambo ambalo
lilimletea uhasama mkubwa sana na viongozi wenzake katika chama chake cha
zamani akiwa Naibu Katibu Mkuu. Zitto alipigana kwa kushirikiana na Wazalendo
wenzake katika Kamati ya Bunge ya PAC na kufanikiwa na hivi sasa vyama vyote
vinakaguliwa na kuweka rekodi nyingine katika nchi nyingi za Afrika. Kwa kazi
hii iliyotukuka Zitto Kabwe amedhibiti fedha za umma kwa vyama vya siasa na
hivi sasa taarifa za mahesabu ya vyama ipo wazi, na tumeona vyama vyote vikiwa
na hati chafu, vikiwemo vyama vya upinzani vya zamani. Ni wajibu wa wanachama
wa vyama hivyo kuwawajibisha viongozi wao wanaogeuza fedha za ruzuku kuwa ni
fedha zao binafsi. Nani anabishia rekodi hiyo ya Kiongozi wetu?
5. KUFUFUA
ZAO LA MKONGE
Mwaka 2012 Zitto Kabwe aliweka rekodi
nyingine tena akiwa mbunge wa kwanza katika Bunge la 10 kuwasilisha Hoja
Binafsi. Aliwasilisha Hoja Binafsini Bungeni akitaka Serikali kufufua Kilimo
cha Mkonge kwa kuwanyanganya wawekezaji wakubwa mashamba waliyobinafsishiwa na
kuyaacha bila kulimwa na badala yake mashamba yale wapewe wakulima wadogo.
Zitto alitaka kubadilisha mfumo wa kulima Mkonge kutoka mashamba makubwa
yanayomilikiwa na tajiri mmoja na kulimwa na manamba mamia na kwenda kwenye
mfumo ambao wakulima wadogo wadogo wanalima Mkonge na hivyo kushirikisha
wananchi wengi zaidi kwenye uchumi wao.
Hoja hiyo ilipingwa na Wabunge kutoka Tanga
lakini iliungwa mkono sana na wananchi wa mkoa huo na hivyo kumwona Zitto kama
mwakilishi wao licha ya kwamba alikuwa akiwakilisha Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Katika Chama chetu ajenda ya kumilikisha
Ardhi wananchi ni ajenda kubwa na ACT Wazalendo kimekua chama cha kwanza nchini
kutangaza kinagaubaga kuwa kitazuia uporaji wa Ardhi na kumilikisha wananchi
ardhi yao wenyewe. Nani anabishia rekodi hiyo?
6. KURASMISHA
KAZI ZA SANAA NA BURUDANI NCHINI
Kwa muda mrefu sana wadau wa tasnia ya
sanaa na burudani nchini walikuwa wanalalamika kazi zao kutokuwa rasmi na hivyo
kuibiwa na mchango wao katika uchumi kutotambuliwa. Mwaka 2012 Zitto Kabwe
akiwa Waziri Kivuli wa Fedha alifanya kampeni maalumu ya kuhakikisha kuwa
wasanii hawanyonywi na kazi zao kutambuliwa rasmi. Aliwasilisha Bungeni
mabadiliko ya Sheria ya Ushuru bidhaa ili kutambua rasmi kazi za sanaa na
burudani na kuhakikisha kuwa wasanii wanalipwa wanavyostahili katika biashara
ya miito ya simu.
Sheria hiyo ilipitishwa na Bunge na Mamlaka
ya Mapato Tanzania ikaanza kutoa stempu rasmi katika CDs za kazi za sanaa ili
kudhibiti wazalishaji kuwanyonya wasanii. Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi wa
Taifa ya mwaka 2015 tasnia ya Sanaa na Burudani imekuwa sekta rasmi ya Uchumi
na imeripotiwa kuwa sasa ina thamani ya shilingi 270 bilioni kama mchango wake
katika Pato la Taifa. Hivi sasa Wasanii wanafaidika maradufu kwa kazi zao
kuuzwa kama miito ya simu na wengine wanapata mamilioni ya shilingi na
kuboresha maisha yao kwa jasho lao. Nani anabisha rekodi hii?
7. KUDHIBITI
UKWEPAJI KODI NA MISAMAHA YA KODI
Wawekezaji kutoka nje wamekuwa wakiibia
nchi yetu kwa kubadilisha badilisha majina ya makampuni yao na kubadili
wamiliki bila ya kulipa kodi hapa nchini. Watanzania mnakumbuka jinsi majina ya
mahoteli makubwa yalivyokuwa yakibadilishwa. Kwa mfano kutoka Sheraton kwenda
Moevenpick na kwenda Serena sasa. Makampuni ya Simu yalivyokuwa yakibadilishwa.
Kwa mfano kutoka Mobitel kwenda Buzz kwenda Tigo.
Vile vile kutoka Celtel kwenda Zain na
kwenda Airtel. Haya yamekuwa yakitokea kwenye maeneo mengi zaidi ya haya. Yote
haya yalitokea bila ya Serikali kupata kodi yeyote. Kwenye mauzo ya Zain kwenda
Airtel Serikali ilipoteza dola za Kimarekani 312 milioni ( zaidi ya shilingi
bilioni 600 kwa bei za sasa za dola ). Kwa uchungu kwa nchi yake Zitto Kabwe
aliwasilisha Bungeni muswada wa sheria wa kurekebisha sheria ya kodi ya Mapato
na kuanzisha tena kodi ya ongezeko la mtaji ( Capital Gains Tax ).
Marekebisho hayo yalipitishwa na Bunge
kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na mwaka huo huo Tanzania ilipata mapato
ya shilingi bilioni 50 kwa mauzo ya Kampuni ya BP kwenda PUMA. Mwaka 2014
Tanzania ilipata dola za kimarekani 222 milioni ( zaidi ya tshs 450 bilioni
)kwa mauzo ya sehemu ya vitalu vya gesi asilia vya kampuni ya Ophir kwenda
kampuni ya Pavilion ya Singapore.
Zaidi ya hapo Zitto na wazalendo wenzake
katika Kamati ya PAC walitoa maagizo ya kuhakikisha kuwa Misamaha ya kodi yote
inakaguliwa na ukaguzi wake kuwekwa wazi ili kudhibiti mianya ya matumizi
mabaya ya misamaha hiyo. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania CAG
anakagua misahamaha ya kodi na PAC iliweka wazi taarifa ya kwanza ya ukaguzi wa
misamaha ya kodi. Nani anabishia rekodi hizi?
8. MABILIONI
YA USWISS
Mwaka 2012 mwezi Novemba Zitto Kabwe
aliwasilisha Bungeni Hoja Binafsi kuhusu mabilioni ya Uswisi ikiwa na lengo la
kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu Watanzania wanaoficha fedha nje ya nchi
kinyume cha sheria. Bunge lilipitisha hoja hii binafsi na kuitaka Serikali
kufanya uchunguzi kuhusu Watanzania wanaotorosha fedha kwenda nje na kuchukua
hatua stahiki za kisheria. Tanzania iliingia katika rekodi ya kuwa nchi ya
kwanza katika nchi za Jumuiya ya SADC kupitisha Azimio la Bunge kuhusu suala la
utoroshaji wa fedha. Licha ya kwamba Serikali haijatoa taarifa yake miaka
miwili sasa toka Azimio la Bunge namba 9 la mwaka 2012, na baada ya danadana ya
muda mrefu kutoka vyombo vinavyohusika Kiongozi wetu Zitto Kabwe ameamua leo
kupasua jipu la hoja hiyo kwa kuweka wazi orodha ya kwanza ya Watanzania 99
wenye akaunti katika Benki ya HSBC ya Uswiss. Uongozi ni umakini, na sio
kukurupuka na kujitafutia sifa za harakaharaka. Ilikuwa ni muhimu Ndugu Kabwe
kufuata taratibu zote kabla ya kuanika majina hayo hadharani. Sasa leo baada ya
kujiridhisha pasipo shaka atayaanika majina hayo hadharani na wale waliokuwa
wanambeza kwamba kashindwa wanyamaze milele! Huyo ndio Zitto, mwenye uvumilivu
na ujasiri usio kifani. Anatenda anayosema. Nani anabisha rekodi hii?
9. KUWAJIBISHA
MAWAZIRI
Katika historia ya Tanzania ni Wabunge
wawili tu walioweza kutoa hoja zilizopelekea Mawaziri wengi kuondolewa
madarakani kwa mpigo. Ni Zitto Kabwe na Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye
aliongoza kamati teule ya Bunge iliyochunguza Mkataba wa kampuni feki ya kufua
umeme ya Richmond. Hoja hii ilipelekea Waziri Mkuu kuwajibika kwa kujiuzulu na
hivyo kumlazimisha Rais wa Jamhuri ya Muungano kuunda upya Serikali kwa kuteua
Waziri Mkuu mwingine.
Zitto ana rekodi ya kipekee. Kwanza mwaka
2012 baada ya Taarifa ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya fedha za umma,
Zitto alikusanya sahihi za wabunge 75 na kuandika hoja ya kutokuwa na imani na
Waziri Mkuu. Shinikizo hili lilipelekea Rais kufukuza kazi mawaziri 8 ambao
Wizara zao zilitajwa kuwa na mahesabu machafu. Pili mwaka 2013 baada ya Kamati
ya Mali Asili na Mazingira kutoa taarifa yake Bungeni kuhusu Operesheni
Tokomeza, Zitto alisimama ndani ya Bunge na kubadilisha mjadala kwa kutaka
Mawaziri wote ambao watendaji wao walitesa wananchi kuwajibika. Mawaziri 4 waliwajibika.
Tatu, mwaka 2014 katika Taarifa Maalumu ya
Kamati ya PAC kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ya Benki ya
Tanzania, Zitto na wazalendo wenzake wa kamati hiyo walipelekea Mawaziri wawili
maarufu kama mawaziri wa Escrow na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika.
Uwajibikaji umekuwa ni ajenda kubwa ya Kiongozi wetu na amekuwa hana aibu hata
kwa watu anaowaheshimu na rafiki zake. Alitaka wawajibike huku akiwatazama
usoni. Ni Viongozi wachache sana wenye ujasiri wa aina hii. Huyu ndio Kiongozi
wa chama chetu cha ACT Wazalendo. Nani anabisha rekodi hii?
10. KUKATAA
POSHO ZA KUKAA
Mwaka 2010 chama chake cha zamani waliweka
katika Ilani yao ya Uchaguzi kupinga posho kama hatua ya kubana matumizi ya
Serikali. Wakakubaliana kuwa wabunge wa chama chao hawatapokea posho ya kukaa
(sitting allowance). Hata hivyo, ilipokuja katika utekelezaji wenzake wote
wakagwaya na Ndugu Zitto Kabwe ni mbunge pekee aliyepinga posho za vikao na
kuzikataa kata kata kwa miaka mitano (5) mfululizo, ambazo ni takribani
shilingi milioni 21 kila mwaka. Katika kipindi hicho cha miaka mitano Zitto
alikaa kuchukua jumla ya Shilingi Milioni Mia Moja na Tano (105,000,000)!!
Kukataa pesa yote hii kwa sababu ya ‘principle’ tu ni jambo nadra sana kutokea
katika mazingira yetu. Zitto anatembea maneno yake. Zitto anatenda anayonena.
Sasa kwa yote hata kwa nini wasimchukie wenye roho zao za kwa nini?
No comments:
Post a Comment