Serikali Yaipiga Faini Ya Bilioni 3 Benki Ya Stanibic Kwa Kuhusika Na Ufisadi wa Dola Milioni 600
Hatua
Ambazo Zimechukuliwa Dhidi Ya Stanbic Bank Tanzania Limited Kuhusu
Ushiriki Wake Kuwezesha Mkopo Wa Serikali Wa Dola Za Kimarekani Milioni
600
____________________
Utangulizi
Mwezi
Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa
shughuli za mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo
na mikopo na pia kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa
Stanbic Bank Tanzania Limited (Stanbic) katika muda mfupi.
Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo.
Ukaguzi
huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47
cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya
Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo ya Ukaguzi wa Benki Kuu
Katika
ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini
miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya
Enterprise Growth Market Advisors (EGMA).
Kampuni
ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa Mkopo kwa
Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa
inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited
kwa pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger).
Malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic.
Jumla
ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani milioni 6, na
zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya
fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
Taarifa
ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa
taratibu, na Benki Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo
kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Aidha,
benki ya Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Financial
Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana
na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama Sheria ya
Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money
Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza
maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
Mnamo
29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya
Uingereza inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa
(Serious Fraud Office - SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti
yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc
ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic Bank Tanzania Limited katika
kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600 kwa Serikali na kwamba
ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma.
Benki
Kuu iliijibu SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu
zinatolewa tu kwa benki au taasisi ya fedha inayohusika, hata hivyo,
Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo
kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
Hatimaye,
Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola
za kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni
7 zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6
zilikuwa ni fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
Kwa
kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia
kutokuweka taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia
Kifungu 67 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeiandikia benki ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3.
Sheria
inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku
ishirini (20) ambacho kitaisha tarehe 30 Januari 2016. Endapo Benki Kuu
haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
Hitimisho
Benki
Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze
kuwa makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa
mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
Aidha,
hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na
makosa ya aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni
uvunjaji wa Sheria za nchi.
Hatua
kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote
itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na Sheria ya
Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
No comments:
Post a Comment