Watendaji Wakuu wa Wakala Wa Vipimo Nchini Wasimamishwa Kazi Kupisha Uchunguzi Wa Upotevu Wa Mafuta Bandarini
SERIKALI
imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo
nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta
bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka
mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza
uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa,
Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na
Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi huo.
“Katibu
Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha
uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi
uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili
kazi ziendelee,” alisema.
Waziri
Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na
polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa
walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na ikithibitika hawakuhusika basi
watarudishwa.
Waziri
Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters
uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.
Jana
(Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow
meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha
akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni.
Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni
12.96/- za sasa).
Pia
Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka
bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya
kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx
Energies.
Katika
ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la
moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini
hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye
maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana
niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili
kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia
wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, FEBRUARI 12, 2016
No comments:
Post a Comment