Waasi Wa Burundi Wakimbilia Nchini Kushawishi Watanzania Wajiunge Na Vikundi Vya Waasi
BAADHI
ya askari waasi wa Burundi, wamebainika kukimbilia nchini na kuanza
kushawishi vijana wajisajili ili wajiunge na vikundi vya waasi.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akifunga Mkutano wa
Pili wa Bunge mjini Dodoma jana na kuwataka wakimbizi na wananchi,
kushirikiana na vyombo vya usalama, kutoa taarifa za uhalifu.
“Kutokana
na ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, kumejitokeza
matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya
wakimbizi ya Nyarugusu.“
"Aidha,
kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na
vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia, imebainika kuwepo
kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida, ambao
wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na vikundi vya
waasi,” alisema Majaliwa.
Pamoja
na changamoto hiyo, ambapo kambi za wakimbizi zilizoko mikoa ya Kigoma,
Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka
mataifa ya Burundi (156,377), Congo-DRC (62,176), Somalia (150) na
mataifa mchanganyiko (192) ikiwemo Rwanda, Uganda, Sudan Kusini na
Ethiopia, hali usalama katika nchi kwa ujumla ni shwari.
Akizungumzia
kuimarisha maadili na utendaji serikalini, Majaliwa alisema Serikali
imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya watendaji wa Serikali na
watumishi wa umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Katika
kuhakikisha watumishi wa umma na Watanzania wote wanafanya kazi,
Mheshimiwa Dk John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amekuja na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.
“Tafsiri
ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali
walizopo, kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe,
urasimu na kutenda kazi kwa mazoea,” alisema.
Alimtaka
kila mwananchi, kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha anafikia malengo
yaliyowekwa na kuwakumbusha watumishi wa umma kuwa, wamepewa dhamana ya
kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Serikali.
Kwa
kuzingatia wajibu huo, amewataka watumishi hao kuhakikisha
wanawahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao na
kuhakikisha kuwa wanatatua kero za wananchi.
Waziri
Mkuu alisema wanatambua kuwa wapo watumishi wanaotekeleza vyema
majukumu yao, lakini pia wapo watumishi ambao hawazingatii maadili ya
kazi zao na pia wanafanya kazi kwa uzembe.
“Serikali
haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasiozingatia
kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa Umma.
"Aidha,
kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, viongozi na watumishi wote
wa umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na kujiamini. Kila
mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki,” alisema.
Kuhusu
dhana ya kutumbua majipu, Majaliwa alisema Rais ametumia dhana hiyo
kusimamia uwajibikaji, hasa kwa wale wenye dalili ya kukosa maadili ya
utumishi wa umma.
“Tafsiri
ya dhana hii ya “Kutumbua jipu” inalenga katika kuwarejesha watumishi
wa umma na walioko serikalini katika mstari mzuri wa utendaji. Nitoe
mwito kwa waheshimiwa wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu
tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita hii kubwa ya ‘Kutumbua
Majipu’.
“Tukiwa
pamoja na kwa kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa nchi ya
maadili na yenye sifa ya juu katika utendaji wa utumishi wa umma,” alisema.
Kuhusu
elimu, Majaliwa alisema tangu Rais Magufuli atoe maelezo ya utekelezaji
wa elimu msingi bila malipo, kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na
ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elimu bila malipo kwa
Watanzania kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne katika shule za
umma.
Alisema
katika mpango huo, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi
atasoma kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne bila ya wazazi na
walezi kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali.
“Hata
hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi
ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari, kalamu
na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa.
“Maeneo
mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi shule, na mahitaji mengine
kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi binafsi. Mzazi au mlezi
ana wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto wake,” amesema.
Kuhusu
elimu ya juu, amesema hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2016, Serikali
ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 207.9 kwa wanafunzi
122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850
ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo.
Kuhusu
uendeshaji wa Bunge, Majaliwa alisema uzoefu alioupata katika muda
mfupi aliokaa pamoja na wabunge Dodoma, amegundua kuwa kuna wabunge
mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali.
Alisema
amebaini wapo wasomi wa ngazi zote, wazee kwa vijana ambao wana uzoefu
na utaalamu mkubwa na kuongeza kuwa wakitumia utaalamu na uwezo mkubwa
walionao katika kuijenga nchi, nchi itapiga hatua.
Aliwataka
wabunge watangulize uzalendo katika kila jambo wafanyalo kwa manufaa ya
Taifa na watu wake, ili nchi ifike mahali ambapo kwa elimu, busara na
hekima na kwa kuacha ushabiki wa kisiasa, watazame mbele katika
kuwaletea wananchi maendeleo.
No comments:
Post a Comment