Monday, February 22, 2016

Uchaguzi wa Marudio Zanzibar: Jecha Adai Maalim Seif Ni Mgombea Halali Na ZEC Haitambui Kujitoa Kwake

Jecha Adai Maalim Seif Ni Mgombea Halali Na ZEC Haitambui Kujitoa Kwake



Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ameibuka tena na kutangaza kukamilika kwa matayarisho ya uchaguzi wa marejeo Machi 20, mwaka huu huku akikataa kutoa majina ya wagombea.

Jecha ambaye tangu afute uchaguzi alionekana hadharani Januari 12, 2016 wakati wa sherehe za Mapinduzi na baadaye kwenye televisheni akitangaza tarehe ya uchaguzi huo wa marudio, alisema wagombea wote ‘waliojitoa’ watapewa haki zote wanazostahiki kupewa kama wagombea kwa kuwa hawakufuata taratibu za kisheria za tume hiyo akimaanisha kuwa hakuna mgombea aliyejitoa kauli ambayo inapingana na msimamo wa CUF ambayo imetangaza kuwa mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif Hamad hatagombea.

Kama alivyofanya wakati anatangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio, jana alizungumza kupitia mwandishi wa Televisheni ya Taifa (TBC), akiwaacha waandishi waliokuwa wameitwa kwa ajili ya mkutano wake nje ya ofisi hiyo.

Jecha ambaye amekuwa haonekani hadharani isipokuwa katika matukio machache, alisema tume yake inawahesabu waliokuwa wagombea katika uchaguzi ulio futwa kuwa ni halali, licha ya kuandika barua za kujitoa katika tume hiyo. 
“Pamoja na kuwa wagombea wengi, hasa wa CUF, kuandika barua za kujitoa katika ofisi za ZEC wilaya na makao makuu, hakuna barua hata moja ambayo imefuata utaratibu wa kisheria na kwa mantiki hiyo, bado tunahesabu wagombea hao ni halali katika uchaguzi mkuu wa marejeo,” alisema Jecha. 
Katika taarifa hiyo, Jecha alisema vyama vinane vimeshathibitisha ushiriki wake katika uchaguzi huo vikiwamo Tadea, ACT, ADC, AFP, SAU, TLP na CCM na utaratibu wa kuwapatia ulinzi wagombea hao umeshaanza. 
Jecha alisema ofisi yake imeshafanya mawasiliano na vyama na wagombea na kuwapa taarifa mbalimbali za matayarisho ya uchaguzi, ili waanze taratibu za kupanga mawakala wao.

Alisema baadhi ya vyama vimetoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa havitashiriki katika uchaguzi, na kuwataka wagombea wao kuandika barua za kutoshiriki katika upigaji kura huo.

“Swala hili naomba nilitolee ufafanuzi kidogo kwa kuwa kauli za vyama hivyo zimewachanganya baadhi ya wagombea waliodhaminiwa na vyama hivyo, ambao bado wanataka kugombea katika uchaguzi huo,” alisema Jecha.

Alisema kila chama cha siasa kilichosajiliwa kinachokusudia kushiriki uchaguzi wa Rais kitawasilisha jina la mgombea wake wa urais kwa tume, na ili mtu awe ameteuliwa kihalali kuwa mgombea urais ni lazima awe amedhaminiwa kwa maandishi na watu wasiopungua 200 ambao wameandikishwa kuwa wapiga kura kutoka kila mkoa wa Zanzibar.

“Kwa bahati mbaya mpaka tunapowasilisha taarifa hii, hakuna chama hata kimoja kati ya vyama ambavyo vimejinadi kuwa havitashiriki katika uchaguzi kilichoiandikia Tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake kushiriki katika uchaguzi,” alisema Jecha katika taarifa yake.

“La pili ni kuwa utaratibu wa kujitoa kwa wagombea katika uchaguzi umefafanuliwa vizuri sana katika kanuni ya uchaguzi ya mwaka 2015,” alisema mwenyekiti huyo akisisitiza kuwa haukufuatwa.

Kwa mujibu wa vifungu hivyo, alisema mgombea wa urais anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa mwenyekiti si zaidi ya saa 10 jioni siku ya uteuzi.

“Mgombea uwakilishi na udiwani anaweza kujiondoa kwa kutoa taarifa ya maandishi aliyoitia saini mwenyewe atakayoiwasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi si zaidi ya saa 10 jioni ya siku inayofuatia siku ya uteuzi."

Jecha alifafanua kuwa tarifa ya kujiondoa chini ya kanuni hizo inatakiwa iambatanishwe na tamko la kisheria lililotolewa na kutiwa saini na mgombeya mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu kwa mgombea wa urais na hakimu kwa mgombea wa uwakilishi au udiwani, mambo ambayo hayakufanyika.

Kuhusu daftari la wapigakura, Jecha alisema kazi ya uchapishaji wa madaftari na vituo vya kupigia kura ndani na nje imeshakamilika, na wanatarajia mwisho wa mwezi huu majina hayo kubandikwa.

Alisema ratiba ya mafunzo kwa wasaidizi na wasimamizi wa majimbo imeshakamilika, na mafunzo hayo kwa Unguja na Pemba yataendeshwa Februari 22-28 na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo watapewa mafunzo Machi 2 hadi Machi 5.

Alisema mafunzo mengine yatakayotolewa ni ya wasaidizi wa vituo vya kupigia kuwa ambayo yamepangwa kufanyika Machi 11 -13 na mafunzo ya mawakala wa uchaguzi siku ya Machi 14 na mafunzo ya walinzi wa vituo vya kupigia kura Machi 15, 2016.

Jecha alisema kazi ya upangaji wa vifaa vya kupigia kura kwa ajili ya kusambazwa wilayani tayari imeanza katika ghala za ZEC za Unguja na Pemba na baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, utaratibu wa kuvisafirisha katika wilaya husika utaandaliwa.

Kuhusu uchapishaji karatasi za kura, mwenyekiti huyo alisema matayarisho yamekamilika baada ya tume kumpitisha mchapishaji wa karatasi hizo.

No comments:

Post a Comment