Mchakato Wa Kura Ya Maoni Ya Katiba Mpya Waanza
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema
mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada ya kumalizika
kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Kauli
hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini wakimtaka Rais
Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala yake mchakato wa
Katiba mpya urudi nyuma baadhi ya mambo yaliyo kwenye Katiba
iliyopendekezwa yarekebishwe.
Itakumbukwa
kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya baadhi ya
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa Serikali Tatu
uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba,
iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Tulikuwa
tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi anavyobeba
mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa tumemaliza (uchaguzi
mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya Maoni),” alisema Jaji Lubuva.
Aliongeza: “Tunaliangalia
na kama Tume tutakuja kuwajulisha wananchi hali ikoje, tuliahirisha
(Kura ya Maoni) ili tumalize hili (uchaguzi mkuu).” alisema Jaji Lubuva na kuongeza.
“Hili
ni suala linalohitaji mambo ya bajeti kubwa na ndiyo tumetoka kwenye
uchaguzi na serikali ndiyo inaanza, kwa hiyo ni suala ambalo
tunaliangalia na baadaye wananchi watajulishwa,” alisema Jaji mstaafu Lubuva.
Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo kwa leo.”
Rais
Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya kulizindua Novemba
20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha mchakato wa
Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia kutokana na
kutokukamilika kwa wakati kwa uandikishaji wapiga kura.
“Napenda
kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo
iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa
maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la
Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu
kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli.
Mbali
na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa walitaka yawe
kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi wa Rais uwe
zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa
mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge, na
muundo mpya wa Bunge la Muungano.
No comments:
Post a Comment