TANESCO Yapeleka Maombi ya Kupandisha Bei Ya Umeme
SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limepeleka maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuomba kupandisha bei ya nishati
hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo ya kushusha bei hiyo.
Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana,
imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka
wadau kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo
utakapoitishwa.
“Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua
uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka
Tanesco,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliwasilisha ombi husika
kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya
mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya
miaka mitatu.
“Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1
kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,”
limeeleza tangazo hilo.
Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo wa
Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea
kusudio lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.
Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza Tanesco, Ewura na Shirika
la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa
bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya umeme
isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta
zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Kutokana na maombi hayo ya Tanesco, Ewura imewataka wadau wa nishati
wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma maoni
yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF
Pensions Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar
es Salaam.
Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa
kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba
(+255-22) 2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe info@energyregulators.org au tovuti http://www. energyregulators. org.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano ya
wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau
mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC);
Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment