Rais Magufuli Asema Yeye si Kichaa wala Dikteta......Aahidi Kuifanyia Mema Nchi hata Akifa awe Rais wa Malaika
Mpekuzi
RAIS
Dk. John Magufuli amesema anapochukua hatua yeye si kichaa, si dikteta,
si shetani wala si mnyama, ila ni mpole, lakini amefika mahali lazima
afanye hivyo kwani ndani ya Serikali yanafanyika mambo ya ajabu.
Kauli
hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika kilele cha Siku ya Sheria
nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa
Mwaka wa Mahakama tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Alisifu
kazi kubwa inayofanywa na Idara ya Mahakama, huku akitangaza uamuzi wa
gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge zaidi ya Sh
bilioni nne ni bora zikawasaidia wananchi.
“Ninapochukua
hatua mimi si mnyama, si dikteta, si shetani, ni mpole kweli, lakini
inafika mahali lazima nifanye, yanayofanyika serikalini ni mambo ya
ajabu sana, nataka kutoa sadaka yangu, inawezekana hata nikifa naweza
kuwa rais wa malaika,” alisema.
Alipongeza
kazi kubwa inayofanywa na mahakama huku akibaki kujiuliza kwanini
katika maadhimisho ya siku yao hawarushi matangazo yao moja kwa moja
kupitia luninga.
“Mnafanya
kazi kubwa, nilipofika niliuliza kwanini hii siku yenu hamrushi ‘live’,
nikajibiwa fedha za kurusha ‘live’ zinapelekwa kuwahudumia wananchi.
“Kipindi
kimoja kurusha ‘live’ kwa wiki mbili inatumika zaidi ya Sh bilioni nne,
ni vizuri kuzikata hizo fedha zinazopelekwa kurusha ‘live’ zikapelekwa
katika kesi za ubunge zinazohitaji shilingi bilioni tatu kusikilizwa
hadi kumalizika kwake,” alisema.
Alisema
mahakama ilikuwa inapewa bajeti ya Sh bilioni 41, lakini mwaka
2015/2016 ilishuka wakatakiwa kupewa Sh bilioni 12 ambazo hadi sasa
hawajapewa.
“Kiongozi
lazima ufikirie wapi pa kupeleka fedha na wapi pa kunyima, watu wa
mahakama mnafanya kazi ya Mungu, nawaahidi ndani ya siku tano nitakuwa
nimewapa Sh bilioni 12 zote.
“Sina
tatizo la masilahi ya wafanyakazi wa mahakama, katika bajeti ya mwaka
huu nitawapa fedha nyingi kuliko bajeti zote zilizopita, fedha zipo,” alisema.
Mahakimu Kutumbuliwa
Rais
Magufuli alisema anamwagiza Jaji Mkuu kuwachukulia hatua mahakimu 502
ambao hawakufikia malengo ya kumaliza kesi 250-260 kwa mwaka. Walimaliza
kesi chini ya 100.
“Mahakimu
ambao hawajafikia kumaliza kesi 260 hayo ndiyo majipu yako Jaji Mkuu,
unatakiwa kuyatumbua, wewe uliniapisha hata mimi, leo unapitisha agizo
mwingine anapinga.
“Unatoa
siku saba sasa sijui ndiyo watamaliza kutoa hizo hukumu, nakuagiza
wachukulie hatua, tusipochukua hatua hakuna kitakachofanyika.
“Walioshindwa
kufikia lengo unawabakiza wa nini, wasomi wako wengi, hata ukitangaza
leo watajitokeza, niruhusu mimi nitangaze, sitaki kuingilia mahakama,” alisema.
Mabilioni ya NIDA
Akizungumzia
hatua yake kwa watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),
alisema ilipewa Sh bilioni 176.6, lakini vitambulisho vilivyotengenezwa
havifiki hata milioni mbili na havina sahihi wakati vitambulisho vya
kupigia kura fedha iliyotolewa haizidi Sh bilioni 70, lakini vina sahihi
za wapigakura wote wa Tanzania ambao ni milioni 23,253,982.
“Utaona
ugumu wa kuongoza, nchi inatawaliwa na madudu ya kila aina, wapo watu
wanacheza na fedha wanavyotaka wakati wapo watu masikini sana, wengine
wanataka bodi zao wakakae Ulaya.
“Hapo
ndipo tulipofikia, wengine wanalipwa mshahara kwa mwezi Sh milioni 35,
naomba mniombee kabla ya kunihukumu, toeni hukumu kwa haki kwa hawa
wanaotaka kuifikisha nchi pabaya, toeni hukumu zao haraka,” alisema.
Kesi za Wakwepa kodi
Rais
Magufuli alisema kuna kesi 442 za kukwepa kodi ambazo zingeamuliwa
Serikali ingepata Sh trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege zaidi
ya sita.
Alimuomba
Jaji Mkuu kuzimaliza kesi 442 na kama zikimalizika fedha hizo Sh
trilioni moja ataipa Idara ya Mahakama Sh bilioni 259 na Sh bilioni 750
zilizobakia zitanunuliwa ndege sita na wafanyafakazi 250 ATCL waliopo
sasa wataondolewa.
Akizungumzia
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisema kuna kesi 26 za watu
waliokutwa na nyara za Serikali, ambazo zipo zaidi ya miaka mitano
hazijaamuliwa kwa sababu upelelezi bado.
“Polisi
wapo, DPP yupo, upelelezi unaendelea kila siku, hapo unaona tatizo
lilipo, DPP upo unapeleleza nini au unatafuta rushwa?” alisema.
Alisema
suala la kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi ya wahujumu uchumi
halihitaji kwenda bungeni kufanya mabadiliko, lifanywe haraka, mahakama
ianze kwani nchi inachezewa.
Pamoja
na hali hiyo Rais Magufuli alikubali kupokea maombi yote yaliyotolewa
na mahakama na kuyazingatia kwani lazima ayaunge mkono ikiwamo kukubali
watumishi wa Idara ya Mahakama wasome na kupatiwa mikopo na Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
“Nimeamua nchi iende na itaenda, anayefikiria ataikwamisha atakwama yeye, nategemea zaidi mahakama katika kufanikisha hilo,” alisema.
No comments:
Post a Comment