Maalim Seif Shariff Hamad Adai Kikwete Ndiye Aliyevuruga Uchaguzi Zanzibar
Mgombea
urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad
amemtuhumu Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuingilia uchaguzi Zanzibar.
Akizungumza
kwenye mkutano wa viongozi wa wilaya na majimbo wa chama hicho
uliofanyika kwenye Ukumbi wa Majid, Kiembe Samaki visiwani Zanzibar
jana, Maalim Seif ambaye ndiye Katibu Mkuu wa CUF alisema, Rais Kikwete
amesababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba.
Alisema,
saa chache kabla ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),
Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo, kituo kikuu cha
kutangazia matokeo kilichokuweko Hoteli ya Bwawani kilizingirwa na
vikosi vya jeshi na polisi na kwamba kitendo hicho kuwa ni “Mapinduzi ya Kikatiba”.
“Aliyekuwa
Amiri Jeshi Mkuu wakati ule alikuwa Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na
ndiye aliyepeleka vikosi vile baada ya kuona chama chake kimeelekea
kushindwa kwa upande wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif na kuongeza;
“Dkt.
Shein wala Balozi Seif (Seif Ali Idd) hawamiliki jeshi wala polisi,
vile ni vikosi vya Dk. Kikwete wakati ule na hawezi kukwepa lawama ya
kuingilia uchaguzi wa Zanzibar.”
Maalim
Seif pia amewashutumu baadhi ya viongozi wakiwemo wa dini wanaojaribu
kupotosha ukweli na kuunga mkono uamuzi batili wa kurejewa uchaguzi
uliotangazwa na ZEC.
Akizungumzia
kuhusu vikao vya kutafuta muafaka wa mkwamo wa kisiasa vilivyokuwa
vikifanyika Ikulu ya Zanzibar, Maalim Seif alisema katika vikao hivyo
walijadiliana na kukubaliana kuwa ZEC imepoteza sifa ya kusimamia
uchaguzi.
Alisema,
ameshangazwa na kitendo cha ZEC kutangaza uchaguzi wa marejeo, huku
viongozi wa CCM walioshiriki mazungumzo hayo wakiunga mkono.
Akizungumzia
hali ya kisiasa Zanzibar, Maalim Seif alisema, siasa za nguvu na
kimabavu zinazoendeshwa na CCM hazitoisaidia Zanzibar na badala yake
zinaweza kuzidisha mgogoro uliopo.
Kauli
ya CUF kugomea uchaguzi uliotangazwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka
huu, imeungwa mokono na viongozi hao wa wilaya na majimbo visiwani humo
wakiwakilisha wananchi na wafuasi wa chama hicho.
Viongozi
hao waliunga mkono hatua hiyo iliyotanguliwa na tamko lililotolewa na
Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho tarehe 28 Januari mwaka huu.
Kwenye
mkutano huo walieleza kuwa uchaguzi halali, huru na wa haki ulifanyika
tarehe 25 Oktoba mwaka jana ambapo wananchi walio wengi walimchagua
Maalim Seif na uchaguzi huo kufutwa bila sababu za msingi.
No comments:
Post a Comment