Tanzania
imedhihirisha kuwa ni tajiri mkubwa wa rasilimali ya gesi asilia baada
ya kugundulika kwa gesi nyingine katika bonde la mto Ruvu yenye ukubwa
wa ujazo wa futi trilioni 2.17.
Ugunduzi
huo wa gesi asilia umefanywa na Kampuni ya Dodsal Hydrocarbons and
Power Tanzania Limited ambayo imekuwa inafanya shughuli za utafutaji wa
gesi na mafuta katika Mkoa wa Pwani.
Mtendaji
Mkuu wa kampuni hiyo, Pilavullathil Surendran alisema jana katika
mkutano wa wawekezaji wa gesi na mafuta ulioandaliwa na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa, thamani ya gesi
iliyoko katika eneo hilo inafikia Dola za Marekani bilioni sita sawa na
Sh trilioni 12.
Ugunduzi huo mpya unafanya hadi sasa Tanzania kuwa na amana ya gesi yenye ukubwa wa futi za ujazo trilioni 57.27.
Kwa
upande wake, Profesa Muhongo alithibitisha kugundulika kwa gesi hiyo
tangu Julai mwaka jana, lakini akaeleza kuwa Serikali imechelewa
kutangaza ugunduzi huo kama inavyoagizwa na Sheria ya Mafuta ya Mwaka
2015 kutokana na shughuli za uchaguzi.
“Sheria
mpya inatutaka kabla ya waziri mwenye dhamana ya gesi kutangaza
ugunduzi mpya wa gesi na mafuta ni lazima athibitishiwe na mamlaka ya
udhibiti wa bidhaa za Petroli na Gesi (PURA).
“Wizara
yangu itawasiliana na mwanasheria mkuu wa serikali ili kupata ushauri
wa kisheria kuhusu jambo hilo na bahati nzuri tayari PURA imeshaanza
kushughulikia jambo hilo na naamini kuwa nitatangaza ugunduzi huo mpya
hivi karibuni,” alifafanua Profesa Muhongo.
Licha
ya ugunduzi huo mpya tayari gesi imegundulika katika maeneo ya kisiwa
cha Songo Songo mkoani Lindi na eneo la Mnazi Bay huko Mtwara na katika
Wilaya ya Mkuranga, Pwani pia kumegundulika kiasi kikubwa cha gesi.
No comments:
Post a Comment