Mbowe Na Zitto Kabwe Wazika Rasmi Ugomvi Wao Wa Muda Mrefu
Uhasama
uliodumu kwa muda mrefu kati ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
(ACT-Wazalendo) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe sasa ni wazi unaonekana kumalizika.
Hali
hiyo inatokana na viongozi hao kwa nyakati tofauti jana kuweka ujumbe
kwenye mitandao yao ya kijamii ya facebook na twitter, ambao unaonyesha
kila mmoja akijutia makosa yake na kutaka waungane kwa ajili ya kutetea
masilahi ya taifa.
Tangu
kuanza kwa mijadala mbalimbali bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita,
Mbowe na Zitto wameonyesha kukubaliana katika misimamo yao na hivyo
kuzua maswali kwamba huenda mbunge huyo wa Kigoma Mjini anataka kujiunga
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mbowe
ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, akiwa na Zitto
wiki iliyopita waliwaongoza wabunge wengine wa Ukawa kususia kikao cha
Bunge kupinga hatua ya Serikali kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya
Bunge kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Baadaye
viongozi hao pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James
Mbatia, waliitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza umma ambavyo
Serikali inarudisha taifa katika zama za udikteta kwa kuzuia haki ya
wananchi kupata habari.
Katika
kikao hicho cha Bunge, Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye, ilitoa taarifa kuwa wanasitisha
matangazo hayo ya moja kwa moja ili kubana matumizi ya Serikali
yanayofikia zaidi ya Sh bilioni nne kwa mwaka.
Katika
ukurasa wake wa facebook na twitter jana, Zitto alinukuu ujumbe wa
Mbowe ambao ulitafsiriwa kwamba ni hatua ya kiongozi huyo wa upinzani
kutaka kumaliza tofauti zake za kisiasa na mbunge huyo.
“Kushirikiana
na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukifanya. Yapo majeraha
mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo huwezi
kuyatibu kwa siku moja. Yapo ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza
kumfanyia mtu kitu kibaya, lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea.
Chochote katika siasa kinawezekana,” aliandika Mbowe.
Jana
kupitia ukurasa wake wa facebook, Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa
Chama cha ACT-Wazalendo, alisema nafasi ya chama chake bungeni ni upande
wa upinzani hivyo atakuwa pamoja na Ukawa.
“Mbowe
siku zote amekuwa kiongozi wangu na siwezi kubeza nafasi yake katika
kujenga demokrasia nchini. Tulipishana, tulikoseana, tusameheane.
“Mimi binafsi siwezi kuwa mfungwa wa magomvi yetu ya miaka ya nyuma. Nilishasamehe walionikosea na kuomba radhi niliowakosea.
“Tunaweza
kupishana kwenye mkakati wa utekelezaji, hatuwezi kupishana kwenye
masilahi ya nchi yetu ya kujenga demokrasia na kukataa udikteta.
“Nafasi
ya ACT-Wazalendo bungeni ni upande wa upinzani, na hivyo tutakuwa na
wenzetu wa upinzani kwenye kujenga hoja zote za kitaifa.
“Mimi
nikiwa mbunge wa ACT-Wazalendo, natekeleza kwa vitendo maelekezo ya
chama kwa kushirikiana na wabunge wenzangu wa upinzani bungeni.
“Chama
chochote makini huweka tofauti binafsi pembeni kwa masilahi mapana ya
taifa. Chama cha ACT-Wazalendo kinaamini katika umoja,” alisema Zitto.
Zitto
alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT-Wazalendo Machi 21, 2015 chama
ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa, lakini ameonekana
kuwa karibu na umoja huo katika vikao vya Bunge la 11 vinavyoendelea
mjini Dodoma.
Mwaka
2013, mwanasiasa huyo machachari pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu Chadema, Profesa Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walifukuzwa kwenye chama hicho, baada ya
mfulululizo wa muda mrefu wa mivutano ya uongozi na baadaye wakaanzisha
chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT) mwaka 2014.
Chadema
ilichukua uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
kutupilia mbali pingamizi la Zitto dhidi ya Kamati Kuu kutojadili
uanachama wake.
No comments:
Post a Comment