Wednesday, March 23, 2016

Zanzibar Yasema Iko Tayari Kufa Njaa Kuliko Kuwanyenyekea Wazungu Wanaoponda Uchaguzi wa Marudio

Zanzibar Yasema Iko Tayari Kufa Njaa Kuliko Kuwanyenyekea Wazungu Wanaoponda Uchaguzi wa Marudio


Licha ya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) kueleza kusikitishwa kwao na uchaguzi wa marudio Zanzibar kufanyika bila kuwapo maelewano ya pande zinazokinzana, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia kushiriki, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema iko tayari kufa njaa kuliko kukubali kuingiliwa uhuru wake.

Juzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyuika Jumapili iliyopita, kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4, hatua iliyozifanya balozi mbalimbali nchini kueleza maskitiko yao na kusisitiza kuwa ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.

Tamko la mabalozi hao lilitolewa na wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani.

Wakati kauli ya mabalozi hao ikizua hofu kuwa huenda Zanzibar na  Tanzania kwa ujumla ikakatiwa misaada na mikopo kutoka nje, kwa madai ya kupindishwa kwa demokrasia, SMZ imetoa msimamo kwamba haitazipigia magoti nchi wahisani na kwamba imeanza kujipanga  kujitegemea kwa mapato ya ndani katika bajeti yake.

Msimamo huo wa SMZ, ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, na Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omary Yusuph Mzee,  walipozungumza  kuhusu msimamo wa EU, Marekani na washirika wao kusikitishwa na kurudiwa uchaguzi kabla ya kupatikana muafaka wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Aboud alisema uchaguzi wa marudio umefanyika Zanzibar ikiwa utekelezaji wa masharti ya katiba na sheria na haikuwa muafaka kwa wahisani kuhoji kufanyika kwake.

“Kitendo wanachokifanya washirika wetu wa maendeleo hakikubaliki katika misingi ya utawala wa sheria. Wanaingilia mambo ya ndani wakati Zanzibar ni nchi huru,”alisema Aboud.

Alisema uchaguzi wa Zanzibar unaendeshwa kwa kufuata masharti ya katiba na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na si maridhiano ya vyama, kama wanavyotaka wahisani.

Aboud alisema Zanzibar iko tayari kushirikiana na washirika wa maendeleo, lakini lazima misaada izingatie utu na heshima ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

“Zanzibar ni nchi huru na itaendelea kuwa huru. Tuko tayari kupokea misaada inayozingatia utu na heshima kwa Zanzibar na wananchi wake kinyume cha hivyo tuko tayari kufa njaa,” alisisitiza.

Naye Mzee kwa upande wake, alisema jana ofisini kwake, Vuga, visiwani hapa kuwa hategemei hilo kutokea katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.

Alisema lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha inaondokana na utegemezi wa wafadhili na kwamba imeanza kuweka mikakati maalum,  kuhakikisha inajitosheleza kwenye bajeti yake.

Alisema miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kufanywa kutimiza lengo hilo ni kuanza kuiga mfumo anaoutumia Rais John Magufuli wa kufuta safari zisizokuwa za lazima kwa viongozi wa serikali.

Aliongeza kuwa mikakati mingine ni kuhakikisha wagonjwa wanaotakiwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, wanapata huduma hiyo nchini kwa kuandaa mipango maalum ya kuleta madaktari.

Mzee ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema Zanzibar inatarajia kutumia mapato yake ya ndani kujitosheleza kwenye bajeti yake.

Alisema Rais Dk. Shein juzi alitoa msimamo wa serikali wa kutaka iwekwe mikakati itakayowezesha Zanzibar kujiendesha kwa bajeti yake bila wafadhili.

Mzee alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za fedha, zikiwamo benki za nje.

Alisema bajeti ya Zanzibar inategemea asilimia 26 hadi28 ya mapato yanayotokana na sekta ya utalii wa ndani na nje na kwamba bado kunahitajika mikakati ili kupanua wigo wa kupata fedha.

Kwa mujibu wa Mzee,  Zanzibar inapokea watalii kati ya 300,000 na  400,000 kwa mwaka na kwamba wanatarajia kuongezeka baada ya kufungua ofisi za kuhamasisha utalii wa nje.

Alisema ofisi maalum za kuhamasisha utalii zimejengwa katika mji wa Mumbai, India na nchini China na kwamba kwa sasa watalii wanatoka moja kwa moja kwao na kufikia Zanzibar.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, Mzee alisema unatarajia kukua kwa asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka na kwamba tofauti za kisiasa zilizopo Zanzibar haziwezi kuathiri mipango ya serikali.

Katika hatua nyingine, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Ali Ameir Mohamed, alisema haikuwa muafaka EU na Marekani kusikitishwa na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.

Alisema ZEC ilikuwa na kila sababu za kuitisha uchaguzi wa marudio ili kukamilisha masharti ya katiba, baada ya uchaguzi wa awali kuvurugika.

Mwanasiasa huyo alisema matatizo ya kisiasa ya Zanzibar yaliachwa na wakoloni wenyewe kutokana na matabaka waliyokuwa wameyajenga kabla ya kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Alisema wahisani jukumu lao kubwa ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika nchi wanazoziwakilisha na si kuingilia mambo ya ndani.

No comments:

Post a Comment