Tuesday, March 22, 2016

Rais Mteule wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein Kuapishwa Kesho Kutwa Alhamis March 24

Rais Mteule wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein Kuapishwa Kesho Kutwa Alhamis March 24


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein zitafanyika siku ya Alhamisi Machi 24 katika uwanja wa Amaan, na maandalizi yote yamekamilika  katika shughuli hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali  akiwemo Rais John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa kitaifa, katika siku hiyo ambayo pia imetangazwa kuwa ni ya mapumziko kwa upande wa Zanzibar ili kuwapa fursa wananchi kuhudhuria kwa wingi katika hafla hiyo.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Bwana Mohamed Aboud katika mahojiano maalum kuhusiana na maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein ikiwa ni siku chache tangu kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.

Waziri Aboud amesema mbali na Viongozi wa kitaifa, Mawaziri wa Serikali zote mbili, Wabunge, Viongozi wa vyama vya upinzani, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, viongozi wa dini na asasi za kiraia pia wamealikwa katika sherehe hiyo itakayofanyika kuanza asubuhi na kumalizika saa saba za mchana.

Akizungumzia kitendawili cha hatma ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Waziri Aboud amesema kuwa mara baada ya kuapishwa kwa Rais mteule, ataunda Serikali yake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

Aidha, Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar hasa wafuasi wa Chama cha Mapinduzi kuendelea kusherehekea ushindi wao bila ya kumbughudhi mtu yoyote na kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu visiwani hapa.

No comments:

Post a Comment