Mabasi yaendayo kasi kuanza ndani ya wiki hii
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
“Wataanza
na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi
huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha
daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya
mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara
ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo
la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa
ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Waziri
Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54,
alitoa jibu hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw.
Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya
usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja.
“Mabasi
yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea
kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,” alisema.
Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema:
“Hivi
sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria
atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita
kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi,
hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”
Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.
No comments:
Post a Comment