Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete awasili Tunisia kusuluhisha mgogoro wa Libya
Rais
Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum
wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya, amewasili jana
Jijini Tunis nchini Tunisia kushiriki Mkutano wa 8 wa Nchi majirani wa
Libya.
Mkutano huo umeitishwa na Serikali ya Tunisia, na ni muendelezo wa jitihada za nchi majirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya.
Rais
Mstaafu Kikwete amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman
alikoshiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa
Jijini Tunis, Jana tarehe 22 Machi, 2016 Dkt. Kikwete amefanya
mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, nchi za Kiarabu na Afrika,
wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini
kwake.
Katika
mazungumzo hayo, Waziri Messaleh amempongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa
kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa
Libya. Amemueleza hali ya usalama na kisiasa ya Libya na mtizamo wa
nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo, na akamhakikishia
ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na
Umoja wa Afrika.
Kwa
upande wake, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru Waziri Abdelkader
Messaleh kwa maelezo yake na ushirikiano aliomuahidi na akamueleza
matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo hasa ikizingatiwa
kuwa nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau
wote kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa.
Rais Mstaafu Kikwete amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.
Katika
ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa nchi
jirani na Libya, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na
Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya,
(Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj, wadau wengine wa
Libya pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya
iliyoko jijini Tunis.
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016.
Imetolewa;
Ofisi ya Rais Mstaafu.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Tunis
22 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment