Maalim Seif Afunguka wakati Wazanzibar wakipiga Kura........"Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM"
Aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad ambaye alitangaza kususia uchaguzi wa marudio licha ya jina
lake kujumuishwa kwenye makaratasi ya kura, amesema ameiachia CCM
kuamua hatma ya nchi hiyo.
Akiongea jana katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam alipotembelewa na Wajumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), wakati uchaguzi wa marudio ukiendelea visiwani Zanzibar, Maalim Seif alisema kuwa CCM ndio walitengeneza hali iliyopo hivi sasa na kwamba ndio wanajua hatma ya uamuzi huo.
“Mimi
sijui [hatma ya Wazanzibar], wauliezeni CCM wao ndio wametengeneza hali
hii… wao ndiyo wamekusudia na wanajua wanaipeleka wapi nchi hii,” alisema Maalim Seif.
“Kilichotokea
Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM ambao pamoja na kwamba
wanafahamu mshindi ni nani katika uchaguzi wa mwaka jana, wameamua
kufanya hicho walichofanya hivi sasa,” aliongeza.
Mwanasiasa
huyo mkongwe ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais amesema kuwa Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha alitumiwa na CCM
kufanya maamuzi na kwamba uamuzi huo umerudisha nyuma maridhiano
yaliyofikiwa miaka mitano iliyopita.
Alisema
kuwa hivi sasa hatazungumza kitu chochote hadi pale matokeo ya uchaguzi
wa marudio yatakapotangazwa lakini akasisitiza kuwa Wazanzibar wanajua
mioyoni mwao Rais wao ni nani.
Jana
wananchi wa Zanzibar wamepiga kura katika uchaguzi wa marudio kufuatia
kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana.
Amani na utulivu vilitawala katika uchaguzi huo ulioshuhudia kuwepo kwa ulinzi mkali.
No comments:
Post a Comment