Wednesday, March 23, 2016

RC Makonda Aitisha Kikao na Walimu ili Kujadili Matatizo Yanayowakabili

RC Makonda Aitisha Kikao na Walimu ili Kujadili Matatizo Yanayowakabili


Mkuu  wa Mkoa  wa  Dar  es  Salaam  Paulo  Makonda  amemwagiza Ofisa Elimu,Raymond  Mapunda  kuitisha  mkutano  wa  walimu  March 26 mwaka  huu ili  kujadili matarizo  yanayowakabili likiwemo  la  kutopanda  madaraja  kwa  wakati.

Makonda  aliyasema  hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akikabidhi  madawati 500 katika shule  ya  msingi  Kawawa yaliyotolewa  na  kampuni  ya  simu  za  mkononi  ya  Tigo.

Mkuu huyo alieleza kuwa yapo matatizo mengi  yanayowakabili walimu yanayotokana  na  watu  wanaojinufaisha matumbo  yao kwa kuwalipa walimu hewa

Katika hatua nyingine,Makonda aliwataka walimu kutovunjwa moyo kutokana na matatizo yaliyopo katika sekta  ya  Elimu.

Naye mkurugenzi wa kampuni ya Tigo,Diego Gutierrez alisema kuwa mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya kampuni ya Tigo kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta  maendeleo ya elimu nchini
==

Zanzibar Yasema Iko Tayari Kufa Njaa Kuliko Kuwanyenyekea Wazungu Wanaoponda Uchaguzi wa Marudio

Zanzibar Yasema Iko Tayari Kufa Njaa Kuliko Kuwanyenyekea Wazungu Wanaoponda Uchaguzi wa Marudio


Licha ya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) kueleza kusikitishwa kwao na uchaguzi wa marudio Zanzibar kufanyika bila kuwapo maelewano ya pande zinazokinzana, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia kushiriki, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema iko tayari kufa njaa kuliko kukubali kuingiliwa uhuru wake.

Juzi, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein, mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyuika Jumapili iliyopita, kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4, hatua iliyozifanya balozi mbalimbali nchini kueleza maskitiko yao na kusisitiza kuwa ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.

Tamko la mabalozi hao lilitolewa na wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Switzerland, Uingereza na Marekani.

Wakati kauli ya mabalozi hao ikizua hofu kuwa huenda Zanzibar na  Tanzania kwa ujumla ikakatiwa misaada na mikopo kutoka nje, kwa madai ya kupindishwa kwa demokrasia, SMZ imetoa msimamo kwamba haitazipigia magoti nchi wahisani na kwamba imeanza kujipanga  kujitegemea kwa mapato ya ndani katika bajeti yake.

Msimamo huo wa SMZ, ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, na Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omary Yusuph Mzee,  walipozungumza  kuhusu msimamo wa EU, Marekani na washirika wao kusikitishwa na kurudiwa uchaguzi kabla ya kupatikana muafaka wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Aboud alisema uchaguzi wa marudio umefanyika Zanzibar ikiwa utekelezaji wa masharti ya katiba na sheria na haikuwa muafaka kwa wahisani kuhoji kufanyika kwake.

“Kitendo wanachokifanya washirika wetu wa maendeleo hakikubaliki katika misingi ya utawala wa sheria. Wanaingilia mambo ya ndani wakati Zanzibar ni nchi huru,”alisema Aboud.

Alisema uchaguzi wa Zanzibar unaendeshwa kwa kufuata masharti ya katiba na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na si maridhiano ya vyama, kama wanavyotaka wahisani.

Aboud alisema Zanzibar iko tayari kushirikiana na washirika wa maendeleo, lakini lazima misaada izingatie utu na heshima ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

“Zanzibar ni nchi huru na itaendelea kuwa huru. Tuko tayari kupokea misaada inayozingatia utu na heshima kwa Zanzibar na wananchi wake kinyume cha hivyo tuko tayari kufa njaa,” alisisitiza.

Naye Mzee kwa upande wake, alisema jana ofisini kwake, Vuga, visiwani hapa kuwa hategemei hilo kutokea katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa.

Alisema lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha inaondokana na utegemezi wa wafadhili na kwamba imeanza kuweka mikakati maalum,  kuhakikisha inajitosheleza kwenye bajeti yake.

Alisema miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kufanywa kutimiza lengo hilo ni kuanza kuiga mfumo anaoutumia Rais John Magufuli wa kufuta safari zisizokuwa za lazima kwa viongozi wa serikali.

Aliongeza kuwa mikakati mingine ni kuhakikisha wagonjwa wanaotakiwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, wanapata huduma hiyo nchini kwa kuandaa mipango maalum ya kuleta madaktari.

Mzee ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema Zanzibar inatarajia kutumia mapato yake ya ndani kujitosheleza kwenye bajeti yake.

Alisema Rais Dk. Shein juzi alitoa msimamo wa serikali wa kutaka iwekwe mikakati itakayowezesha Zanzibar kujiendesha kwa bajeti yake bila wafadhili.

Mzee alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za fedha, zikiwamo benki za nje.

Alisema bajeti ya Zanzibar inategemea asilimia 26 hadi28 ya mapato yanayotokana na sekta ya utalii wa ndani na nje na kwamba bado kunahitajika mikakati ili kupanua wigo wa kupata fedha.

Kwa mujibu wa Mzee,  Zanzibar inapokea watalii kati ya 300,000 na  400,000 kwa mwaka na kwamba wanatarajia kuongezeka baada ya kufungua ofisi za kuhamasisha utalii wa nje.

Alisema ofisi maalum za kuhamasisha utalii zimejengwa katika mji wa Mumbai, India na nchini China na kwamba kwa sasa watalii wanatoka moja kwa moja kwao na kufikia Zanzibar.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, Mzee alisema unatarajia kukua kwa asilimia 8 hadi 10 kwa mwaka na kwamba tofauti za kisiasa zilizopo Zanzibar haziwezi kuathiri mipango ya serikali.

Katika hatua nyingine, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi,  Ali Ameir Mohamed, alisema haikuwa muafaka EU na Marekani kusikitishwa na kufanyika kwa uchaguzi wa marudio.

Alisema ZEC ilikuwa na kila sababu za kuitisha uchaguzi wa marudio ili kukamilisha masharti ya katiba, baada ya uchaguzi wa awali kuvurugika.

Mwanasiasa huyo alisema matatizo ya kisiasa ya Zanzibar yaliachwa na wakoloni wenyewe kutokana na matabaka waliyokuwa wameyajenga kabla ya kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Alisema wahisani jukumu lao kubwa ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika nchi wanazoziwakilisha na si kuingilia mambo ya ndani.

CCM na CUF Watwangana Ngumi Pemba Wakati Wakisherehekea Ushindi wa Dr. Shein

CCM na CUF Watwangana Ngumi Pemba Wakati Wakisherehekea Ushindi wa Dr. Shein


Jeshi la Polisi jana walitumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya amani baada ya wananchi kuanza kupigana kwa sababu za kisiasa wakati wakisherehekea ushindi wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, katika kijiji cha Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni, Pemba.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid Salim, alidai vurugu hizo zimesababishwa na wanachama wa CCM kutoka katika kijiji cha Kwale wilayani humo.

Alisema baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa marudio, wanachama wa CCM katika kijiji cha Kwale, walianza kukusanyika na ngoma zao na kuanza safari ya kuingia katika kijiji cha Mjini Wingi, sehemu ambayo ni ngome ya wanachama wa CUF, huku wakisherehekea kwa kurusha 'vijembe' (maneno ya kejeli) na matusi.

“Pamoja na kutakiwa kuacha matusi wakati wakisherehekea ushindi wa Dk. Shein, waliendelea na kusababisha wenzao kupandwa na ghadhabu kuwachemka na kuanza kupigana,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, wanachama wa CCM kutoka kijiji cha Kwale, walilazimika kukimbilia Kituo cha Polisi Micheweni.

Alisema askari walipofika eneo la tukio, walianza kupiga mabomu ya kutoa machozi na kuvunja milango ya nyumba.

Mwenyekiti huyo alisema nyumba 15 zilivunjwa milango wakati wakiwasaka watu waliokuwa wakihusishwa na vurugu hizo ambazo zilianza kufanyika saa 10:00 jioni na kuendelea hadi usiku juzi.

Aidha, alisema kwa mujibu wa mabaki ya milipuko, jumla ya mabomu 27 yanadaiwa kupigwa mbali na nyumba kuvunjwa milango na kusababisha watu zaidi ya 28 kuyakimbia makazi yao katika kijiji hicho.

“Watu wanne wamekamatwa akiwamo mtoto mwenye umri wa miaka 13, lakini wananchi wengi wamekimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa cha Kojani na Maziwang'ombe,” alisema Rashid.

Hata hivyo, alisema jambo la kushagaza polisi wameamua kuwakamata watu waliofanyiwa fujo badala ya kuwakamata waliokuwa chanzo cha vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba watu watano wanashikiliwa kwa uchunguzi wa kuhusika na tukio hilo.

Hata hivyo, alikanusha kuvunjwa milango 15 pamoja na kutumika mabomu 27 kurejesha hali ya utulivu baada ya wananchi kuanza kupigana.

Waliokamatwa katika mkasa huo ni Kombo Khalfan Faki, Salim Hassan Khamis, Mjawiri Faki, Khatib Dawa Juma na Assaa Bakar Ali, wakazi wa kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis Othman, alisema hali katika kijiji hicho imerejea kuwa ya kawaida na kuwataka wananchi kuendelea na sherehe za kumpongeza Dk. Shein bila ya kuvunja sheria.

Alisema wananchi waliokimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa cha Kojani na Maziwang'ombe, watakuwa ndiyo waliohusika na vurugu na kwamba raia mwema hana sababu ya kukimbia askari.

Tuesday, March 22, 2016

Chidi Benz Apelekwa Bagamoyo Sober House Kwa ajili Kumsaidiwa Kuacha Matumizi ya Madawa ya Kulevya

Chidi Benz Apelekwa Bagamoyo Sober House Kwa ajili Kumsaidiwa Kuacha Matumizi ya Madawa ya Kulevya

Meneja wa Diamond, Babutale akishirikiana na Kalapina wamemchukua Chidi Benz na kumpeleka Life and Hope Rehabilitation Organization iliyopo Bagamoyo kwa ajili kumsaidiwa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya.

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibuni rapa huyo kuomba msaada baada ya kuona ameshindwa kukabiliana na matatizo ya kiafya ambayo yamekuwa yakimkabili.

Kupitia instagram, Babutale amepost video na kuandika:

"Mwana amekubari kukaa Soba ila anasisitiza wana mje kumtembelea kumpa hope na kuleta mapokopoko manjari. Mungu bariki hii safari ya matumaini"

Katika video hiyo Babu Tale alisema wamefika salama Life and Hope Rehabilitation Organization, Huku Kalapina akiomba mungu kumsaidia Chidi Benz.


CUF Yatangaza Kutoyatambua Matokeo ya Uchaguzi wa Marudio Zanzibar....Pia Haitambui Ushindi wa Dr Shein

CUF Yatangaza Kutoyatambua Matokeo ya Uchaguzi wa Marudio Zanzibar....Pia Haitambui Ushindi wa Dr Shein


Kufuatia ubakaji wa demokrasia kupitia kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio uliofanywa juzi tarehe 20 Machi, 2016, jana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alikamilisha kazi aliyoagizwa kwa kutangaza kile alichokiita matokeo ya uchaguzi wa Urais.

Chama Cha Wananchi (CUF) kilishaeleza msimamo wake kuhusu ubakaji huo wa demokrasia kupitia taarifa yake kiliotoa tarehe 18 Machi, 2016. Baada ya hatua ya jana tunaweka msimamo wetu kwamba:

1. Hatutambui hicho kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi, 2016 na kwa maana hiyo hatumtambui huyo aliyedaiwa kuwa mshindi na kwa msingi huo huo hatutoitambua wala kushirikiana na Serikali itakayoundwa kutokana na matokeo hayo batili ya uchaguzi batili.

2. Tunawapongeza kwa dhati Wazanzibari wote kwa ukomavu wao mkubwa wa kisiasa waliouonesha kwa kuitikia wito wa mpendwa wao Maalim Seif Sharif Hamad na chama chao cha CUF na kutoshiriki katika uchaguzi huo batili. Kwa ujasiri wao huo wameudhihirishia ulimwengu kwa njia za amani na za kistaarabu kwamba chaguo lao ni Maalim Seif Sharif Hamad. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameyathibitisha maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya kupitia uchaguzi huru na wa haki wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

3. Tunavipongeza vyombo vya habari vya ndani na nje na jumuiya ya kimataifa kwa kuonesha hali halisi ilivyokuwa na jinsi Wazanzibari walivyoikataa CCM, walivyowakataa watawala na walivyokataa kutumika kubaka demokrasia. Wazanzibari wameandika historia nyengine mbele ya macho ya ulimwengu. Kwa mara nyengine tena Wazanzibari wameshinda.

4. Tunajua Wazanzibari wana hamu ya kujua hatua zinazofuata katika kusimamia maamuzi yao ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015. Chama chao kinawatoa wasiwasi Wazanzibari kwamba hakijayumba na kinafuatilia haki yao hiyo kwa njia za amani na za kidemokrasia na kitakuwa kikiwaeleza kila kinachoendelea.

HAKI SAWA KWA WOTE

NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU – CUF
22 Machi 2016

Rais Mteule wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein Kuapishwa Kesho Kutwa Alhamis March 24

Rais Mteule wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein Kuapishwa Kesho Kutwa Alhamis March 24


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein zitafanyika siku ya Alhamisi Machi 24 katika uwanja wa Amaan, na maandalizi yote yamekamilika  katika shughuli hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali  akiwemo Rais John Pombe Magufuli pamoja na viongozi wengine wa kitaifa, katika siku hiyo ambayo pia imetangazwa kuwa ni ya mapumziko kwa upande wa Zanzibar ili kuwapa fursa wananchi kuhudhuria kwa wingi katika hafla hiyo.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Bwana Mohamed Aboud katika mahojiano maalum kuhusiana na maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mteule wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein ikiwa ni siku chache tangu kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.

Waziri Aboud amesema mbali na Viongozi wa kitaifa, Mawaziri wa Serikali zote mbili, Wabunge, Viongozi wa vyama vya upinzani, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, viongozi wa dini na asasi za kiraia pia wamealikwa katika sherehe hiyo itakayofanyika kuanza asubuhi na kumalizika saa saba za mchana.

Akizungumzia kitendawili cha hatma ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Waziri Aboud amesema kuwa mara baada ya kuapishwa kwa Rais mteule, ataunda Serikali yake kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.

Aidha, Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar hasa wafuasi wa Chama cha Mapinduzi kuendelea kusherehekea ushindi wao bila ya kumbughudhi mtu yoyote na kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu visiwani hapa.

Mabasi yaendayo kasi kuanza ndani ya wiki hii

Mabasi yaendayo kasi kuanza ndani ya wiki hii


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo kasi (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.

“Wataanza na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 22, 2016) wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.

Waziri Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa jibu hilo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Bw. Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja. 
“Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi taxi ni gharama kubwa,” alisema.

Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: 
“Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”

Alisema tatizo la usafiri kwa wafanyabiasha wa feri litakwisha hivi karibuni baada ya mabasi hayo kuanza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MACHI 22, 2016.

Tuhuma za Rushwa: Hussein Bashe Naye Ajiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Bunge

Tuhuma za Rushwa: Hussein Bashe Naye Ajiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Bunge


Mbunge wa Nzega Mjini na Kiongozi wa chama cha CCM, ameishtumu Kamati ya Huduma za Jamii anayohudumu kuwa kuna baadhi ya Wajumbe wammepokea rushwa.

Kutokana na shtuma hizo ameamua kuungana  na  Zitto Kabwe  kumuandikia spika  barua  ya kujiuzulu  na kumtaka achunguze na kuchukua hatua.

Hii  ni nakala ya barua yake aliyomwandikia spika wa bunge

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete awasili Tunisia kusuluhisha mgogoro wa Libya

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete awasili Tunisia kusuluhisha mgogoro wa Libya

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya, amewasili jana Jijini Tunis nchini Tunisia  kushiriki Mkutano wa 8 wa Nchi majirani wa Libya.

Mkutano huo umeitishwa na Serikali ya Tunisia, na ni muendelezo wa jitihada za nchi majirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya.

Rais Mstaafu Kikwete amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman alikoshiriki Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.

Akiwa Jijini Tunis, Jana tarehe 22 Machi, 2016 Dkt. Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Maghreb, nchi za Kiarabu na Afrika, wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh, aliyemtembelea hotelini kwake.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Messaleh amempongeza  Rais Mstaafu Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa Libya. Amemueleza hali ya usalama na kisiasa ya  Libya na mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo, na akamhakikishia ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.

Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete amemshukuru Waziri Abdelkader Messaleh kwa maelezo yake na ushirikiano aliomuahidi na akamueleza matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo hasa ikizingatiwa kuwa nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau wote kuhakikisha mgogoro huo unatatuliwa.

Rais Mstaafu Kikwete amesisitiza kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Libya liko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.

Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa nchi jirani na Libya,  Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya,  (Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj,  wadau wengine wa Libya  pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya iliyoko jijini Tunis.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016.

Imetolewa;
Ofisi ya Rais Mstaafu.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
Tunis
22 Machi, 2016

Spika Wa Bunge Mh.ndugai Afanya Mabadiliko Ya Baadhi Ya Wajumbe Wa Kamati Za Kudumu Za Bunge

Spika Wa Bunge Mh.ndugai Afanya Mabadiliko Ya Baadhi Ya Wajumbe Wa Kamati Za Kudumu Za Bunge



==

Zitto Kabwe Atangaza Kujiuzulu Ujumbe Kamati ya Huduma Za Jamii Baada ya Wajumbe wake Kutuhumiwa Kwa Rushwa

Zitto Kabwe Atangaza Kujiuzulu Ujumbe Kamati ya Huduma Za Jamii Baada ya Wajumbe wake Kutuhumiwa Kwa Rushwa


Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, ameishtumu Kamati ya Huduma za Jamii anayohudumu kuwa kuna baadhi ya Wajumbe wammepokea rushwa.

Kutokana na shtuma hizo ameamua kumuandikia spika  barua  ya kujiuzulu  na kumtaka achunguze na kuchukua hatua.

Hii  ni nakala ya barua yake aliyomwandikia spika wa bunge

UKAWA Washinda Umeya wa jiji la Dar es Salaam....Wamepata Kura 84, CCM Kura 67

UKAWA Washinda Umeya wa jiji la Dar es Salaam....Wamepata Kura 84, CCM Kura 67


Hatimaye uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam umekamilika leo katika ukumbi wa Karimjee, na kushuhudia Isaya Mwita wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Mwita ameibuka na ushindi na kutangazwa kuwa Meya Mpya wa Jiji la Dar es Salaam baada ya kupata kura 84 akimshinda mpinzani wake, Yenga Omary  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 67.

Uchaguzi huo umeweka historia ambapo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi (1992), Chama Cha Upinzani kimepata nafasi ya kuongoza jiji hilo.

Uchaguzi huo uliahirishwa mara kadhaa kutokana na mvutano uliokuwa unaibuka kati ya wajumbe wa CCM na Chadema na kuzua vurugu wakati mwingine.

Tofauti na ilivyo kwa tarehe nyingine za uchaguzi zilizopangwa na kuahirishwa wakati wajumbe wakiwa ukumbini, viongozi wa ngazi za juu wa Chadema pamoja na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa walihudhuria kushuhudia uchaguzi huo.
==

Monday, March 21, 2016

Breaking News: Dr. Ali Mohammed Shein Atangazwa Rasmi kuwa Mshindi wa Kiti Cha Urais Zanzibar Kwa Asilimia 91.4

Breaking News: Dr. Ali Mohammed Shein Atangazwa Rasmi kuwa Mshindi wa Kiti Cha Urais Zanzibar Kwa Asilimia 91.4

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar  Jecha Salim Jecha amemtangaza Rasmi Mgombea urais wa CCM Dr. Ali Mohammed Shein kuwa  mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar akiwa na kura 299.982  sawa  na  asilimia  91.4.
==> Matokeo yote kama yalivyotangazwa  yako  hapo  chini....

Baadhi Ya Matokeo ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza La Wawakilishi Zanzibar

Baadhi Ya Matokeo ya Uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza La Wawakilishi Zanzibar


Matokeo ya uchaguzi wa marudio uliofanyika jana visiwani zanzibar kwa upande wa wajumbe wa baraza la wawakilishi yameanza kutangazwa kisiwani pemba.
 
1.Jimbo la Chakechake aliyeshinda ni Suleiman Said wa CCM
2.Jimbo la Ole mshindi ni Musa Ali Musa wa CCM
3.Jimbo la Wawi mshindi ni Hamad Ali Rashid wa CCM
4.Jimbo la Ziwani mshindi ni Asaa ali Hamad wa UPDP
5.Jimbo la Chonga aliyetangazwa mshindi ni Shaibu Ali wa CCM

Matokeo ya awali ya Urais kwa Majimbo ya OLE, Ziwani, Chonga, Wawi na Chake Yanaonyesha Dr. Ali Mohamad Shein Anaongoza

Matokeo ya awali ya Urais kwa Majimbo ya OLE, Ziwani, Chonga, Wawi na Chake Yanaonyesha Dr. Ali Mohamad Shein Anaongoza



Mwandishi Salma Said Apatikana Baada ya Watekaji Kumuachia Huru

Mwandishi Salma Said Apatikana Baada ya Watekaji Kumuachia Huru


Siku tatu baada ya mwandishi wa Mwananchi na DW, Salma Said kutoweka, jana alipatikana baada ya kukutwa katika Hospitali ya Regency ya jijini Dar es Salaam  na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kuhojiwa.
Habari zilizopatikana jana jioni na kuthibitishwa na mumewe, Ali Salim Khamis na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi, Simon Siro zilisema Salma alisajiliwa jana mchana katika hospitali hiyo.
Ali aliyekuwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alisema kwa ufupi kuwa amepata taarifa hizo na kufika Dar es Salaam kuzifuatilia. 
Kamanda Siro alisema ni kweli Salma amepatikana na ametumwa mkuu wa upelelezi wa kanda hiyo kumfuata hospitali ampeleke kituoni kwa mahojiano. 

“ Tumefungua jalada la uchunguzi wa tukio hili juzi,” alisema Sirro na kuongeza. 
“Wapelelezi walizungumza na mume wa Salma na kuna mambo amewaeleza lakini hatuwezi kuyaweka wazi kwa sasa, hadi uchunguzi utakapokamilika, tumeipata namba ya simu aliyowasiliana nayo na mumewe akiwa huko kunakoaminika amefichwa,” alisema. 
 
Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika tamko lake ililolitoa jana ilieleza kuwa kutekwa kwa mwanahabari huyo kumezua maswali mengi kwa wananchi, familia yake, wadau na wanahabari wa ndani ya nchi na wale wa jumuia za kimataifa.
“Kutekwa kwa Salma kunatokana na kazi yake ya uanahabari, ndiyo maana ushahidi wa awali uliopatikana kwa njia ya ujumbe wa sauti ukiwa na sauti inayoaminika kuwa ni yake, ulieleza wazi kutekwa kwake kunatokana na yeye kuripoti dosari zinazoendelea katika uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Joseph Mbilinyi, Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo wa Kambi ya Upinzani. 
 
Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) alidai kuwa matukio mbalimbali yanayoendelea Zanzibar yakiwamo ya matumizi ya nguvu, vitisho na hata vitendo vya kikatili dhidi ya wanaosimamia haki, vinaendelea kuitia Serikali ya CCM doa, Taifa na dunia nzima.

Maalim Seif Afunguka wakati Wazanzibar wakipiga Kura........"Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM

Maalim Seif Afunguka wakati Wazanzibar wakipiga Kura........"Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM"


Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alitangaza kususia uchaguzi wa marudio licha ya jina lake kujumuishwa kwenye makaratasi ya kura, amesema ameiachia CCM kuamua hatma ya nchi hiyo.

Akiongea jana katika Hotel ya Serena Jijini Dar es Salaam alipotembelewa na Wajumbe wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA), wakati uchaguzi wa marudio ukiendelea visiwani Zanzibar, Maalim Seif alisema kuwa CCM ndio walitengeneza hali iliyopo hivi sasa na kwamba ndio wanajua hatma ya uamuzi huo.

“Mimi sijui [hatma ya Wazanzibar], wauliezeni CCM wao ndio wametengeneza hali hii… wao ndiyo wamekusudia na wanajua wanaipeleka wapi nchi hii,” alisema Maalim Seif.

“Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM ambao pamoja na kwamba wanafahamu mshindi ni nani katika uchaguzi wa mwaka jana, wameamua kufanya hicho walichofanya hivi sasa,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais amesema kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha alitumiwa na CCM kufanya maamuzi na kwamba uamuzi huo umerudisha nyuma maridhiano yaliyofikiwa miaka mitano iliyopita.

Alisema kuwa hivi sasa hatazungumza kitu chochote hadi pale matokeo ya uchaguzi wa marudio yatakapotangazwa lakini akasisitiza kuwa Wazanzibar wanajua mioyoni mwao Rais wao ni nani.

Jana wananchi wa Zanzibar wamepiga kura katika uchaguzi wa marudio kufuatia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana. 
Amani na utulivu vilitawala katika uchaguzi huo ulioshuhudia kuwepo kwa ulinzi mkali.