Aliyemtishia Nape kwa bastola sio polisi- Waziri Mwigulu
Waziri
wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema mtu aliyemtishia kwa bastola
aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye si
askari wa Jeshi la Polisi, lakini ameshapatikana na atashughulikiwa kwa
mujibu wa utaratibu wa ulinzi na usalama.
Mwigulu
alisema hayo baada ya kufungua mkutano wa kazi wa mwaka wa maofisa
waandamizi wa polisi, makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi wa Jeshi la
Polisi ambao unafanyika mjini hapa.
“Ameshapatikana
(aliyemtishia Nape) na atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za ulinzi
na usalama ambazo zimekuwa zikifanyika ndani, lakini
hazitangazwi,”alisema.
Hata
hivyo, Mwigulu alikataa kuelezea kwa undani kuhusu mtu huyo kwa
kubainisha anatoka taasisi gani wala jina la mtuhumiwa kwa madai kuwa ni
kwa sababu ya usalama wake.
Baadhi ya taasisi za ulinzi na usalama nchini ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Usalama wa Taifa na Takukuru.
Mtu
huyo alifanya kitendo hicho wakati Nape, ambaye alikuwa Waziri wa
Habari, alipokuwa anaelekea Hoteli ya Protea alikopanga kuzungumza na
waandishi wa habari baada ya mbunge huyo wa Mtama kuachwa katika
mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.
Mtu
huyo alikuwa pamoja na wenzake wawili ambao kwa pamoja walikuwa
wakimlazimisha arudi kwenye gari lake na kuondoka, lakini Nape alibisha
na ndipo mtu huyo aliporudi nyuma, kuchomoa bastola kutoka kiunoni na
kisha kumtishia kabla ya kutulizwa na mwenzake.
Watu hao walitoweka eneo hilo muda mfupi baadaye.
Siku moja baada ya tukio hilo Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kumtafuta mtu huyo.
Mwigulu aliandika katika ukurasa wake wa twitter akisema:
“Mh
Nape sio jambazi, hana record za uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola
si cha Kitanzania na si cha kiaskari. Nimemuagiza IGP achukue hatua.”
Tukio
hilo lilitokea siku chache baada ya RC Paul Makonda kuvamia kituo cha
televisheni cha kampuni ya Clouds Media, akiwa na askari wenye silaha za
moto na kulazimisha arekodiwe mahojiano baina ya watangazaji wa kipindi
cha Shirika la Wambeya Duniani (Shilawadu) na mwanamke anayedai kuzaa
na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye
ameibukia kuwa mpinzani wa kiongozi huyo.
Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kuhusu askari hao waliojumuika kufanikisha uvamizi huo.
No comments:
Post a Comment